DIWANI wa Kata ya Puni Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Mhandisi Jumanne Rajabu, ametaja kero sita kuu zinazowakabili wananchi wa Kijiji cha Nyanshimbi ambazo amesema ataanza kuzifanyia kazi katika kipindi chake cha uongozi wa miaka mitano.
Kero hizo ni pamoja na ukosefu wa maji safi na salama, ukarabati wa barabara korofi, ukosefu wa huduma ya umeme katika ngazi ya vitongoji, uboreshaji wa miundombinu ya elimu ikiwemo chakula kwa wanafunzi shuleni, upungufu wa watumishi na vifaa tiba katika zahanati, pamoja na kufufua josho la kuoshea dawa za mifugo.
Diwani Rajabu, ametaja vipaumbele hivyo jana alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyanshimbi katika mkutano wa hadhara, wa kuwashukuru kwa kumchagua kuwa diwani wao katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29 mwaka huu, na kumpigia kura nyingi za ushindi Rais Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Itwangi Azza Hillal Hamad.
Amesema baada ya kuapishwa rasmi kuwa Diwani, alifanya ziara katika vijiji vyote vitatu vinavyounda Kata ya Puni, kwa lengo la kubaini changamoto zinazowakabili wananchi, na kwamba katika Kijiji cha Nyanshimbi ameona ni sahihi kuanza na kero hizo sita kutokana na uzito wake kwa maisha ya kila siku ya wananchi.
“Ndugu zangu wananchi wa Kijiji hiki cha Nyanshimbi, Mkutano wangu huu nimekuja leo kusema Asante kwa kunipigia kura nyingi na kunichangua kuwa diwani wenu, na kura nyingi kwa Rais Samia Suluhu Hassan, na Mbunge wa Itwagi Azza Hillal Hamad,”amesema Mhandisi Rajabu.
Amesema llicha ya asante hiyo, lakini ataanza na vipaumbele hivyo sita ambazo ni kero kubwa kwa wananchi wa kijiji hicho, na atakuwa akizitatua kwa awamu awamu sababu maendeleo ni hatua kwa hatua, kisha ataendelea na zingine.
Aidha, amewasihi pia wananchi kuendelea kudumisha Amani ya nchi, na kwamba wasikubali kutumika kuivuruga kwa maslahi ya watu wachache, sababu vita ni adui wa maendeleo. Naye Katibu wa Siasa na Uenezi (CCM) Mkoa wa Shinyanga Richardi Masele, amewashukuru wananchi hao kwa kumpigia kura nyingi za ushindi Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Mbunge wa Itwangi Azza Hillal Hamad na Diwani wa Puni Mhandisi Jumanne Rajabu kwamba kuchagua mafiga hayo matatu watapata maendeleo ya kweli.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED