Waziri Chande: Jitazameni mtaishi vipi na jamii

By Godfrey Mushi , Nipashe Jumapili
Published at 11:29 AM Dec 14 2025
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande.
PICHA: GODFREY MUSHI
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande.

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande, amewapa ushauri wa bure, vijana wanaohitimu katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka kilichoko Moshi, mkoani Kilimanjaro, kutumia elimu waliyoipata kutambua wataishi vipi na jamii.

Chande, amewaeleza kuwa, vyeti tu havitoshi, bali utekelezaji wa yale waliyojifunza na kufunzwa chuoni, waende wakaonyeshe kwa vitendo huko wanapokwenda, kwa sababu cheti ni karatasi. Naibu Waziri huyo, amewafunda vijana hao jana , wakati wa mahafali ya 61 ya chuo hicho.

 “Tumieni vyema taaluma yenu kufanya kazi kwa weledi na ufanisi mkubwa katika kuisaidia jamii kutatua changamoto zinazowakabili, ikiwemo kusaidia kutatua migogoro baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu. Vyeti tu havitoshi, bali utekelezaji wa yale mliyojifunza na kufunzwa chuoni, hivyo  nendeni kuyaonyesha kwa vitendo huko mnapokwenda, kwa sababu cheti ni karatasi lakini maarifa mliyoyapata katika kutambua mnaishi vipi na jamii, nchi na rasilimali zinazokuzunguka hilo ndio muhimu kuliko zote.”

1


Aidha, Waziri Chande, amekitaka chuo hicho kutanua wigo wa kada za masomo, ikiwemo masomo ya muda mfupi katika fani za kuongoza watalii, huduma kwa wateja na udereva, ili kutanua wigo kwa vijana kusomea masomo hayo.
“Anzeni sasa, ili kusudi vijana hao wanapokuwa wanakwenda kuongoza watalii, wawe na taaluma yao vizuri. Mtalii avutike mara nyingine kurudi na waweze kuelezea vizuri vivutio vyetu tulivyonavyo, lakini pia waweze kuwa sehemu ya usalama wa vivutio vyetu na nchi yetu…Jambo hilo litasaidia kuongeza idadi wa watalii katika nchi yetu,”alisema Chande.

Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka, Prof. Julius Nyahongo, amesema kuwa udahili wa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2024/2025, umeongezeka kwa asililimia 10 ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi waliohitimu mwaka uliopita.