Rais TAHLISO: Tuiombee nchi yetu amani iendelee kutawala

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 06:28 PM Dec 14 2025
Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Vyuo na Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO)  Geofrey Kiliba
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Vyuo na Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO) Geofrey Kiliba

Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Vyuo na Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO) Geofrey Kiliba amewataka Watanzania hasa vijana kuwa makini dhidi ya matendo na maamuzi ya wanaharakati, akiwahimiza kulinda, kuombea na kudumisha amani na mshikamano wa nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili, Jijini Dar es Salaam, Kiliba amesisitiza kuwa ikiwa mambo yatakwenda tofauti na amani na mshikamano ukapotea nchini, watakaoathirika ni Watanzania wote wakiwemo Vijana wenye wajibu wa kulinda na kuidumisha amani iliyopo.

"Ninaomba kila Kijana, Kila Mtanzania, walau ndani ya siku yake moja, atumie walau dakika moja mpaka tatu, kuombea amani, ulinzi na mshikamano ndani ya nchi yetu. Sisi Wakristo tunaamini na maandiko yanasema Bwana asipoulinda Mji waulindao wanakesha bure." Amesema Kiliba.

Kiliba pia amewataka Watanzania kuchukua wajibu wa kuwashauri  wanaharakati kwa lugha ya upendo na kuwaeleza athari za matendo wanayoyafanya na kuyahamasisha nchini, akiwataka Watanzania kuwafuata kwenye mitandao yao ya kijamii na skuwaeleza umuhimu wa amani na athari za matukio ya uvunjifu wa amani wanayoyahamasisha.