Wakati Serikali ikiweka wazi dhamira ya kufanya mabadiliko ndani ya jeshi la polisi ili kulisogeza jeshi hilo karibu na wananchi kama chombo muhimu kwao, wadau wametaka kuzingatiwa kwa mapendekezo yanayotolewa kwa lengo la mabadiliko katika jeshi hilo.
Huku tayari pakiwapo mapendekezo ya tume ya haki jinai baada ya kufanya kazi na kutoa ripoti yake tangu mwezi Julai mwaka juzi, mapendekezo hayo yanaendana kwa kiasi kikubwa na yale ya wadau wengine ikiwemo vyama vya siasa, taasisi za dini na asasi za kiraia.
Katika ripoti ya Tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman iliyotolewa Mwezi Julai mwaka juzi, tume hiyo ilibaini masuala kadhaa yanayolalamikiwa kuhusu jeshi la polisi nchini ikiwamo suala la ukamataji watuhumiwa, maadili na rushwa, utunzaji wa vielelezo vya watuhumiwa na matumizi mabaya ya madaraka.
Katika suala la ukamataji watuhumiwa tume hiyo ilibainisha kuwa vyombo vyenye mamlaka ya kukamata, mara nyingi hutumia nguvu kubwa kupita kiasi na kusababisha mateso kwa watuhumiwa jambo ambalo linaungwa mkono na wadau wengine ikiwemo vyama vya siasa ambavyo ni mojawapo ya wahanga katika hilo.
Katika mojawapo ya mapendekezo yake tume ilipendekeza mamlaka husika zichukue hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi (polisi na wengineo) wanaokiuka taratibu za kazi ya ukamataji na uhifadhi wa watuhumiwa.
Eneo lingine ambalo tume ilibaini mapungufu ni katika suala la utunzaji wa vielelezo vya watuhumiwa tume hiyo ilibaini kuwa utunzaji wa vielelezo katika baadhi ya vituo vya polisi vilivyotembelewa na Tume hauzingatii ipasavyo miongozo na sheria.
“Vituo vya Polisi vinakabiliwa na ufinyu wa nafasi ya kuhifadhi vielelezo na hakuna umakini wa kutosha miongoni mwa watendaji katika utunzaji wa vielelezo. Hali hii inachangia Jamhuri kushindwa mashauri mahakamani kwa sababu ya kuharibika kwa vielelezo.”
“Aidha, kuharibika au kupotea kwa vielelezo huisababishia Serikali hasara kwa kulipa fidia pale amri inapotolewa ya kurejesha vielelezo tajwa kwa mmiliki wake.” imesema sehemu ya ripoti hiyo
Matumizi mabaya ya madaraka ni mojawapo ya malalamiko makubwa ya wadau kuhusu jeshi la polisi na hata katika ripoti hiyo ya Jaji Chande suala hilo lilibainishwa, tume ilibaini vyombo vilivyo na mamlaka ya kukamata (ikiwamo jeshi la polisi) vikitumia vibaya mamlaka yake ya ukamataji na hivyo kusababisha bughudha na kero kwa wananchi. Mathalan, kukamata watu bila sababu na kukamata watu kwa makosa ya madai. Kutokana na kuwekwa mahabusu bila sababu za msingi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED