DC ahimiza malezi bora kwa watoto

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 03:30 PM Dec 28 2025
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam, Saad Mtambule
PICHA: MTANDAO
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam, Saad Mtambule

JAMII imetakiwa kuhakikisha watoto wanalelewa katika misingi ya upendo, amani, kufanyakazi na kuwa mchango wa kuimarisha amani na mshikamano nchini.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam, Saad Mtambule katika kongamano la kidini lililofanyika  jijini Dar es Salaam kujadili amani, ustawi na maendeleo ya jamii na taifa.

 "Tujiulize ni mara ngapi katika wiki na mwezi tumekaa baba, mama na watoto tunasoma vitabu vyetu vya dini, tukatafakari mafundisho, “ alisema na kuongeza kuwa: “ Mara ngapi tumekaa na vijana tukazungumza masuala yanayowahusu wao, Taifa na familia juu ya kuimarisha upendo, amani, kufanya kazi na kuwa na mchango kwenye Taifa letu. “

 Alisisitiza kuwa kama jamii, baba, mama na walezi wakiweza kufanya hayo,  amani na upendo utakuwepo na matukio mengine ya rushwa na uhalifu kupungua. Alielezea  umuhimu wa familia kukaa, kujadili, kusoma na kutafakari maandiko matakatifu, namna ya kuimarisha amani, upendo na kuwa na mchango katika Taifa wa kutatua changamoto za kijamii na kisiasa nchini.