Wenye mahitaji maalum wapatiwa bajaji

By Julieth Mkireri , Nipashe Jumapili
Published at 02:12 PM Jan 11 2026
Wenye mahitaji maalum wapatiwa bajaji
Picha: Julieth mkireri
Wenye mahitaji maalum wapatiwa bajaji

Watu wenye mahitaji maalum katika Mtaa wa Muheza, Kata ya Mailimoja, Manispaa ya Kibaha, wameishukuru Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, kwa kuwapatia mkopo wa bajaji, unaolenga kutatua kero ya ukosefu wa kipato cha uhakika katika maisha ya kila siku.

Wakizungumza baada ya kukabidhiwa bajaji hizo Januari 9. 2026 wamesema kuwa awali walikuwa hawana chanzo cha uhakika cha kipato, hali iliyokuwa ikiathiri ustawi wa familia zao. 

Wamesema kupitia mkopo wa asilimia 10 uliotolewa na Halmashauri, changamoto hiyo imepata ufumbuzi na sasa wanakwenda kujiimarisha kwenye eneo la uchumi na kuondokana na utegemezi .

Aidha, Abubakari Sebastian Swai na Christopher Severin ambao ni kati ya wanufaika wa mkopo huo wamemshukuru Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dk. Rogers Shemwelekwa, kwa kuwapatia mkopo huo wa bajaji ambao utaongeza uwezo wao wa kujitegemea kiuchumi. 

Kupitia mkopo huo wameahidi kurejesha  kwa wakati ili kutoa fursa kwa wengine wenye uhitaji kunufaika na mpango huo.

Watu hao wenye ulemavu watatu kutoka mtaa wa Muheza wamekopeshwa bajaji zenye thamani ya shilingi milioni 40.5, fedha ambazo zinatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwao na familia zao.