Miongo inayobeba matumizi lugha ya matusi mitihani kitaifa nini chanzo?

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 03:54 PM Jan 11 2026
AI
Picha: AI
AI

Kwa miongo kadhaa taarifa kwenye vyombo vya habari, zinazohusu baadhi ya wanafuzni kutumia lugha ya matusi kwenye karatasi za kujibia mitihani kitaifa, zimekuwa zikijirudia.

Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), mwisoni mwa wiki, limetangaza matokeo ya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne na Kidato cha Pili uliofanyika Oktoba na Novemba, 2025.

Wanafunzi 173,015 hawajafanya upimaji huo, huku matokeo yote ya wanafunzi 89 yakifutwa kwa udanganyifu na kuandika matusi.

Kati ya matokeo yaliyofutwa 41 ni waliofanya udanganyifu na wanane walioandika matusi kwenye scripti zao za Upimaji wa Kitaifa Darasa la Nne na kwa Kidato cha Pili waliofanya udanganyifu ni 29 na 11 walioandika matusi kwenye scripti katika upimaji huo.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Prof. Said Mohamed,  alitoa taarifa hiyo mwishoni mwa wiki, ambapo amesema  yanahusisha wanafunzi waliopimwa kwa kuzingatia mifumo miwili ya mitaala. Amesema katika upimaji wa kitaifa wa Darasa la Nne 2025 wanafunzi wote wamefanya upimaji kwa mitaala iliyoboreshwa.

Amesema kati yao ambao hawajafanya upimaji huo,  Darasa la Nne ni wanafunzi 93,309 sawa na asilimia 5.89, Kidato cha Pili ni wanafunzi 77,689 sawa na asilimia 8.74 na wanafunzi wa Kujitegemea ni 2,017 sawa na asilimia 21.33.

Prof. Mohamed amesema katika Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili 2025 wanafunzi wa mtaala wa awali walifanya upimaji kwa mtaala huo. “Wanafunzi waliokuwa wakitumia mtaala ulioboreshwa (Mkondo wa Amali)  walitahiniwa kwa mara ya kwanza kwa kuzingatia mtaala ulioboreshwa,"amesema.

Prof. Mohamed amesema kwa mwaka 2026 wanafunzi wote wa Kidato cha Pili watapimwa kwa mtaala ulioboreshwa.

je, sababu ni ipi kwa baadhi ya wanafunzi kutumia lugha ya matusi kwenye karatasi za kujibia mitihani kitaifa, ambazo zimekuwa zikijirudia?