Kwa mvuto wake wa kipekee, uthubutu na uwezo wa kujiweka karibu na wananchi wa kawaida, nyota wa muziki Bobi Wine, ametingisha siasa za Uganda.
Tangu abadilishe mwelekeo wa taaluma yake kuelekea siasa, takribani muongo mmoja uliopita, kijana huyo mwenye umri wa miaka 43, amekuwa mwiba mkubwa kwa Rais Yoweri Museveni, mwenye umri wa miaka 81, ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 40.
Bobi Wine, amewavutia na kuwachochea maelfu ya vijana wa Uganda, kundi linalounda sehemu kubwa ya idadi ya watu wa nchi hiyo.
Akiwa amekulia katika mitaa duni ya mji mkuu wa Kampala, alijiita rais wa geto na anafanya kampeni zake akilenga masuala kama ukosefu wa ajira kwa vijana na haki za binadamu.
Januari 15, mwaka huu, Bobi Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Ssentamu, atakabiliana na Rais Museveni katika uchaguzi wa urais kwa mara ya pili. Hata hivyo, nafasi yake ya ushindi inaonekana kuwa ndogo.
Tangu aingie kwenye siasa, mwanamapinduzi huyu anayejitambulisha mwenyewe amewahi kufungwa na kukabiliwa na mashtaka kadhaa ya jinai.
Mateso yake yamevuta hisia za dunia nzima, mwaka 2018 wanamuziki maarufu akiwamo Chris Martin wa Coldplay na Damon Albarn wa Gorillaz, walisaini ombi la kumtaka aachiliwe kutoka kizuizini.
Bobi Wine, alikamatwa kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume cha sheria, lakini kesi hiyo ilionekana na wengi kuwa na msukumo wa kisiasa. Baadaye pia alikamatwa kwa tuhuma za uhaini, lakini hatimaye kesi zote hizo zilifutwa.
"Mimi ndiye mgombea niliye karibu zaidi na wananchi," aliiambia BBC alipokuwa akiendesha kampeni kuelekea uchaguzi huo.
"Ndiyo maana miongoni mwa wagombea wanane, mimi ndiye anayefuatiliwa zaidi, ninayenyanyaswa zaidi na ninayehofiwa zaidi."
Mamlaka zimekuwa zikikanusha mara kwa mara kuwa kukamatwa kwa Bobi Wine, pamoja na wafuasi ama wanachama wa chama chake cha National Unity Platform (NUP), kunahusiana na siasa. Zinasema kuwa vizuizi vyovyote vilifanyika ili kudumisha sheria na utulivu.
Rais pia amemtuhumu Bobi Wine kwa kuandaa mikutano yenye vurugu katika maeneo yenye makazi ya watu wengi, akihatarisha usalama wa wafuasi wake na wananchi kwa ujumla tuhuma ambazo zimekanushwa na kiongozi huyo wa upinzani.
Museveni alipoingia madarakani mwaka 1986, Bobi Wine alikuwa karibu kutimiza miaka minne tu. Museveni na jeshi lake la waasi, National Resistance Army (NRA), walikuwa wametwaa madaraka kupitia mapambano ya silaha.
Babu yake Bobi Wine, Yozefu Walakira, alikuwa sehemu ya kundi jingine la waasi, lakini mara kwa mara wakati wa mgogoro huo alimkaribisha Museveni nyumbani kwake.
Bobi Wine alitumia sehemu kubwa ya utoto wake mjini Kampala. Mama yake, Margaret Nalunkuuma, muuguzi, alikuwa ndiye tegemeo kuu la familia na alimlea katika eneo aliyoinunua katika mtaa duni wa Kamwokya.
Akiwa kijana, Bobi Wine alianza kupenda sanaa. Alisoma katika Chuo Kikuu maarufu cha Makerere nchini Uganda, ambako alipata stashahada ya muziki, dansi na maigizo mwaka 2003.
Alikutana na mke wake na mama wa watoto wake wanne, Barbara "Barbie" Itungo, akiwa mwanafunzi na wote walishiriki katika igizo moja.
Baada ya chuo kikuu, Bobi Wine alianza rasmi kazi ya muziki, akiuita mtindo wake "edutainment" yaani burudani yenye elimu. Moja ya nyimbo zake za awali kabisa, Kadingo, ilikuwa kuhusu usafi binafsi.
Muziki wake, unaochanganya reggae, Afrobeats na midundo ya asili ya Uganda, ulipata umaarufu mkubwa na ulimjenga kama mtetezi wa mabadiliko ya kijamii na kisiasa.
Licha ya umaarufu wake kuendelea kukua, Bobi Wine alichagua kuendelea kurekodi muziki katika studio aliyojenga mwenyewe katika mtaa wa Kamwokya. Pia alifanya kazi kama muigizaji.
Mwaka 2016, wanamuziki wengi maarufu nchini humo walimuunga mkono Rais Museveni katika uchaguzi wa kurejea madarakani. Bobi Wine, hata hivyo, alikataa.
Alitoa wimbo uitwao Situka, ambapo alitafakari akisema:
"Wakati mambo yanapokuwa magumu, walio imara lazima wasimame imara hasa pale viongozi wanapogeuka kuwa wapotoshaji na walezi wanapogeuka kuwa watesaji."
Mwaka uliofuata, Bobi Wine aliingia rasmi kwenye siasa.
Aliwania ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kyadondo Mashariki kama mgombea huru, akiwakabili wanasiasa kutoka chama tawala cha NRM na FDC, ambacho wakati huo kilikuwa chama kikuu cha pili kwa ukubwa nchini Uganda.
Alishinda kwa kishindo kikubwa, akipata kura zaidi ya mara tano ya mpinzani wake wa NRM.
Katika kipindi hicho, Bobi Wine alianzisha harakati za Peoples' Power, kundi lililokuwa likipigania demokrasia bora na hali nzuri za kijamii.
Wanachama wake walianza kuvaa kofia nyekundu, ambazo hadi leo zimebaki kuwa alama ya utambulisho wa kiongozi huyo wa upinzani.
Baada ya kuzuiwa mara kadhaa kusajili People Power kama chama cha siasa, Bobi Wine alijiunga na chama kidogo kilichokuwa tayari kimesajiliwa cha NURP.
Baadaye chama hicho kilibadilisha jina na kuitwa National Unity Platform (NUP) na Bobi Wine akachaguliwa kuwa kiongozi wake.
Ifikapo mwaka 2021, alikuwa tayari kumpinga Museveni katika uchaguzi wa urais. Katika kipindi cha kuelekea uchaguzi huo, watu kadhaa waliuawa, wengi wao wakiaminika kupigwa risasi na vikosi vya usalama.
Hatimaye Bobi Wine alishindwa katika uchaguzi huo, akipata asilimia 35 ya kura dhidi ya asilimia 59 za Museveni.
Miaka miwili baadaye, simulizi ya maisha ya kiongozi huyo wa NUP iliandikwa katika filamu ya National Geographic iliyopewa jina Bobi Wine: The People's President. Filamu hiyo ilisambazwa duniani kote na hata kupata tuzo za Oscar.
Licha ya umaarufu wake wa kimataifa na mafanikio katika filamu, msimamo wa kisiasa wa Bobi Wine haujabadilika sana tangu alipovuma takribani muongo mmoja uliopita.
Anaendelea kujivunia asili yake ya unyenyekevu na kampeni zake bado zimejikita kwenye masuala kama rushwa, ukosefu wa ajira kwa vijana na usambazaji wa haki wa rasilimali.
Hata hivyo, kuna wasiwasi kwamba endapo, kinyume na matarajio, angekuwa rais, historia yake binafsi huenda ikawa changamoto.
Jeshi lina ushawishi mkubwa katika siasa za Uganda kwa kuzingatia kwamba limewahi kuwaondoa au kujaribu kuwaondoa madarakani viongozi kadhaa tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 1962.
Kwa kuwa Bobi Wine hana historia ya kijeshi wala uzoefu wa uwaziri na badala yake alitokea kwenye sekta ya ubunifu na sanaa, huenda ikawa vigumu kwa majeshi kumchukulia kwa uzito kama rais.
Hata hivyo, ni mtazamo ambao yeye mwenyewe anaukataa. Huu ni mtazamo ambao yeye mwenyewe anaukataa.
"Uganda imekuwa tayari kwa kiongozi wa kiraia tangu zama za kale," anasisitiza, akiongeza kuwa kwa mujibu wa katiba ya Uganda, jeshi linapaswa kuwa chini ya mamlaka ya kiraia.
Katika kipindi cha kuelekea siku ya kupiga kura, Bobi Wine amekuwa akifanya kampeni kote nchini, mara nyingi akiwa amevaa koti la kujikinga na risasi pamoja na kofia ya chuma.
Picha na video zinaonesha wafuasi wake wakiandamana na msafara wake, wakikabiliana na gesi ya kutoa machozi na mipigo ya maji iliyotumiwa na vikosi vya usalama.
Katika kituo kimoja kaskazini mwa Uganda, wanaume waliovalia sare waliwachapa wafuasi wa Bobi Wine kwa fimbo walipokuwa wakitengeneza ngao ya kibinadamu kumlinda kiongozi huyo wa upinzani.
Licha ya hatari ya vurugu, wafuasi wake wanaendelea kuwa imara na wenye kujitolea, wakijaza mikutano ya kampeni bila kuyumbishwa.
Naye Bobi Wine hakati tamaa. "Uchaguzi huu ni kuhusu ukombozi," anasema. "Ni kuhusu uhuru, ni kuhusu wananchi kudai na kutumia sauti zao. Tunawaomba watu wajitokeze na kuandamana kupitia sanduku la kura."
Chanzo: BBC
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED