Mikononi mwa Polisi akisingizia kajifungua, kaibiwa mtoto

By Julieth Mkireri , Nipashe Jumapili
Published at 03:35 PM Jan 11 2026
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase
Picha: Julieth Mkireri
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, linamshikilia Agnes Liku, (35) mkazi wa Kijiji cha Mwanzomgumu, Kata ya Msimbu Wilaya ya Kisarawe, kwa kutoa taarifa za uongoOkuwa amejifungua mtoto katika zahanati ya kijiji hicho na mtoto kuchukuliwa na ofisa tabibu asiyefahamika.

Akielezea kuhusiana na tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amesema Januari 6, 2026 saa 12 jioni, Agnes alisema alienda katika zahanati hiyo ya kijiji akiwa na rafiki yake Eveline Mazigo.

Kamanda Morcase amesema Agnes alifika katika zahanati hiyo akieleza ana uchungu wa kunifungia ambapo Afisa Tabibu Tatu Nyahoza alimpokea na kumpima.

Hata hivyo alipopimwa Agnes alibainika kuwa njia ya uzazi haijafunguka kuruhusu mama huyo kujifungua.

Kwa mujibu wa Kamanda Morcase saa tatu usiku walifika ndugu Maduki Shabani na Catherine Raphael walifika katika zahanati hiyo kumsaidia Agnes ambaye alijieleza kwamba anasubiri kujifungua.

Ilipofika saa saba usiku Agnes anaelezwa kwamba aliwaita ndugu akiwa chumba cha kujifungulia na kuwaeleza kwamba amejifungua na tabibu aliyemhudumia ameondoka na mtoto.

Ndugu walimuita tabibu Tatu Nyahoza aliyekuwa chumba cha jirani ambaye alimpima tena Agnes na kubaini njia bado haijafunguka kuruhusu kujifungua isipokuwa aliona damu.

Tabibu Tatu alivyoona sintifahamu hiyo aliamua kutoa taarifa kwa uongozi wa Kitongoji kisha Jeshi la Polisi kupitia Polisi Kata ya Msimbu.

Kamanda Morcase amesema Polisi walifika wakiwa na wataalamu wa matukio kufanya mahojiano na mashahidi kisha kumpeleka Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe kwa vipimo zaidi.

Amesema katika Hospitali ya Wilaya, madaktari bingwa wa akinamama walifanya vipimo vyote na kubaini hakukuwa na dalili za Agnes kuwa mjamzito wala kujifungua.

Kufuatia taarifa hiyo polisi wamekamilisha upelelezi wa jalada hilo na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.