Misri, Nigeria, Morocco na Senegal zimejihakikishia kucheza nusu fainali ya mataifa ya Afrika, AFCON, baada ya mechi za robo fainali kukamilika Jumamosi usiku.
Wenyeji Morocco watacheza na Nigeria, huku Senegal, ambao walikuwa wa kwanza kutinga nusu fainali, wakicheza dhidi ya Misri.
Mechi zote mbili zitachezwa Jumatano ya wiki hii.
Mabingwa mara saba Misri walishinda nafasi ya mwisho katika nne bora baada ya kuwatoa mabingwa watetezi Ivory Coast kwa kuwachapa mabao 3-2 katika mchezo wa kusisimua Jumamosi usiku, na kumaliza utawala wa Tembo hao na sasa watawakabili Senegal.
Mapema katika mashindano hayo, Senegal tayari walikuwa wamejihakikishia nafasi yao baada ya ushindi mgumu wa 1-0 dhidi ya Mali, bao la Iliman Ndiaye katika kipindi cha kwanza likionekana kuwa la muhimu katika mchezo mkali wa dabi ya Afrika Magharibi.
Simba wa Teranga walionesha ukomavu wao wa mashindano kwa kudhibiti mchezo na kulinda faida yao ya bao moja ili kufikia nusu fainali nyingine ya AFCON.
Wenyeji Morocco pia wanabaki imara katika njia ya kutwaa taji la kwanza kwa kipindi cha miaka 50 baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Cameroon mjini Rabat.
Mabao kutoka kwa Brahim Diaz na Ismaël Saibari yaliwahakikishia Simba wa Atlas hao kuendelea kampeni yao ya kuvutia nyumbani.
Wao Nigeria waliichapa Algeria mabao 2-0 mjini Marrakech kwa mabao ya Victor Osimhen aliyefunga kwa kichwa na Akor Adams.
Matokeo yanasisitiza tofauti ndogo katika hatua hii ya mashindano, ambapo asili na utulivu vimeleta tofauti.
Baada ya awamu isiyotabirika ya makundi na raundi ya 16 bora yenye ushindani mkali, robo fainali iliashiria mahali ambapo uzoefu ulianza kujitokeza.
Nusu fainali itachezwa Jumatano ya Julai 14, huku Senegal ikikabiliana na Misri na Morocco ikikabiliana na Nigeria, kabla ya fainali yake kupigwa mjini Rabat, Julai 18.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED