WAKATI Rais Samia Suluhu Hassan akituma salamu za faraja kwa Simba na Yanga baada ya kuondolewa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, uongozi wa Yanga umewasilisha rasmi malalamiko yake katika Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuhusiana na maamuzi ya mchezo wao uliochezwa kwenye Uwanja wa Tshwane-Loftus Versfeld jijini Pretoria, Afrika Kusini.
Yanga imeondolewa katika michuano hiyo kwa penalti 3-2 na wenyeji, Mamelodi Sundowns wakati Simba iliaga michuano hiyo kwa kukubali kufungwa magoli 2-0 na Al Ahly ya Misri.
Katika malalamiko yao, Yanga inadai ilifunga bao halali dakika ya 57 kupitia mchezaji wake, Aziz Ki Stephane (aliyevaa jezi namba 10), lakini likakataliwa na waamuzi waliochezesha mechi hiyo wakiongozwa na Dahane Beida kutoka Mauritania.
Yanga inadai Beida na wasaidizi wake waliokuwa katika VAR, Daniel Ayi kutoka Ghana na Jerson Dos Santos wa Angola, kwa sababu zao walikataa kupitia marejeo na kwa kufanya hivyo walikiuka kanuni za matumizi ya teknolojia hiyo jambo ambalo halikuwa sahihi na haki kwenye mpira wa miguu.
Yanga pia inadai matukio mbalimbali yaliyokuwa yanafanywa na mwamuzi huyo wa kati yalikuwa na viashiria vya upangaji matokeo katika mchezo huo wa robo fainali ikiwamo kutotoa adhabu ya kadi nyekundu kufuatia faulo aliyofanyiwa mchezaji wake akiwa anaelekea kufunga.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara pia wanalalamikia hakukuwa na haki kwenye uamuzi na kutilia shaka weledi wa mwamuzi huyo wa Mauritania.
Yanga inaiomba CAF kufanya uchunguzi kutokana na matukio mbalimbali ili kubaini yalifanyika kwa makosa ya kibinadamu au yalilenga upangaji wa matokeo.
Yanga imeweka wazi imelazimika kuwasilisha malalamiko yake kwa kufuatia Kanuni ya 16 (3) ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ya CAF.
Naye Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, ametupa lawama zake kwa Beida akidai aliwapendelea wenyeji.
Gamondi amesema ni mbeleko ya chuma ndiyo iliyowapeleka Mamelodi Sundowns hatua ya nusu fainali na si vinginevyo.
“Tumecheza na timu kubwa, vijana wamepambana, tumetengeneza nafasi na kushindwa kuzitumia, tumecheza vizuri, ila hahitaji hata msaada wa VAR kujua kama lilikuwa bao au la, tulistahili kupewa, nimesikitishwa na maamuzi ya waamuzi wa mchezo.
Mwamuzi hataki kuangalia VAR? Labda kuogopa watu wakubwa. Tunarejea nyumbani kujiandaa na michezo iliyopo mbele yetu,” amesema Gamondi.
"Mchezo mzuri Yanga. Mmeonyesha kiu na juhudi ya kuiletea heshima nchi yetu hadi kufikia hatua hii. Tunatarajia makubwa zaidi kutoka kwenu kwenye mashindano haya ya Ligi ya Mabingwa ya Shirikisho la Soka Afrika msimu ujao. Tutaendelea kuwaunga mkono na kuwapa motisha," ameandika Rais Samia.
Kipa wa Mamelodi Sundwons, Ronwen Williams, ambaye aliokoa penalti nne katika mechi moja ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mapema mwaka huu akiwa na Afrika Kusini, aliibuka tena shujaa kwa kuokoa penalti mbili zilizopigwa na Aziz Ki na Dickson Job, huku ile ya Ibrahim Hamad 'Bacca', ikipaa.
Waliofunga penalti za Yanga ni Augustine Okra na Joseph Guede.
Penalti za Mamelodi ziliwekwa wavuni na Marcelo Allende, Lucas Ribeiro, Neo Maema, huku kipa wa Yanga, Djigui Diarra akipangua penalti ya Leandro Siniro.
Kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, Misri, Simba iliondolewa katika michuano hiyo baada ya kufungwa mabao 2-0 na mabingwa watetezi, Al Ahly.
Mabao ya Al Ahly katika mechi hiyo iliyowafanya wasonge mbele kwa ushindi wa jumla wa magoli 3-0 yaliwekwa wavuni na Amr El Solia na Mahmoud Karhaba.
Baada ya mechi hiyo iliyochezwa kuanzia saa 5:00 usiku, Rais Samia pia akawafariji akiandika tena kwenye akaunti yake ya instagram.
"Mchezo mzuri Simba. Usiku haukuwa wa ushindi lakini tumeziona juhudi na zinatupa faraja na matarajio kuwa, msimu ujao wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa ya Shirikisho la Soka Afrika mambo yatakuwa mazuri zaidi. Ahadi yetu ni kuendelea kuwaunga mkono na kuwapa motisha." Yalikuwa ni maneno ya kuwatia moyo wawakilishi hao ambao ni mara ya pili mfululizo wakitolewa hatua hiyo, msimu uliopita wakitolewa dhidi ya Wydad Casablanca kwa penalti 4-3.
Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha, amesema hakuna wa kulaumiwa katika hilo kwa sababu wachezaji wake wamepambana kwa uwezo wao wote, lakini wameshindwa kupata mabao na Al Ahly licha ya kucheza nyumbani, lakini walipaki basi na kushambulia mara chache, hatimaye wakapata walichokihitaji.
"Tumepambana, lakini hatukufanikiwa, hii ni timu kubwa sana Afrika, inahitaji zaidi ya hiki tulichonacho, hakuna wa kulaumiwa, nadhani msimu ujao tutarudi tukiwa imara zaidi ya hivi," amesema kocha huyo.
Timu hizo sasa zinarejea nchini kuendelea na mechi zao za Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Kombe la FA.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED