Shule ya Bethsaida yaomba wafadhili kuisaidia

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 05:39 PM Oct 19 2025
MKUU wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bethsaida ya watoto  Yatima na waishio katika mazingira Magumu Erasto Emmanuel akizungumza wakati wa  Mahafali ya 17 ya Kidato cha Nne yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya shule hiyo Mpiji Magoe
PICHA: MPIGAPICHA WETU
MKUU wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bethsaida ya watoto Yatima na waishio katika mazingira Magumu Erasto Emmanuel akizungumza wakati wa Mahafali ya 17 ya Kidato cha Nne yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya shule hiyo Mpiji Magoe

SHULE ya Sekondari Bethsaida imewaomba wafadhili kujitokeza kwa wingi kusaidia uendeshaji wa shule hiyo ambayo inahudumia watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu.

Akizungumza wakati wa mahafali ya Kidato cha Nne yaliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Shule hiyo, Bw. Erasto Emmanuel, alisema shule hiyo inategemea zaidi misaada ya wafadhili, hasa kutoka nje ya nchi, lakini idadi yao imepungua kutokana na changamoto za dunia ikiwemo mlipuko wa ugonjwa wa Corona na vita kati ya Urusi na Ukraine.

“Kupungua kwa wafadhili kulianza mwaka 2020 kipindi cha Korona, na vita kati ya Urusi na Ukraine vimechangia kupunguza zaidi uwezo wao wa kutusaidia,” amesema Bw. Emmanuel.

Alifafanua kuwa kupungua kwa wafadhili kumesababisha udahili wa wanafunzi kushuka, kwani sasa analazimika kuchukua idadi ndogo ya watoto wanaoweza kuhudumiwa kwa rasilimali zilizopo.

1
Aidha, alitoa wito kwa wadau na wafadhili kujitokeza kufadhili watoto mmoja mmoja au kusaidia mahitaji muhimu kama chakula, vifaa vya kujifunzia na mishahara ya walimu ili shule iweze kujiendesha bila wasiwasi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shule hiyo, Bw. Raymond Machary, amesema shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma ambapo wanafunzi wengi wanaomaliza wamekuwa wakichaguliwa kuendelea na masomo katika shule mbalimbali za sekondari nchini.

2

“Mwaka jana wanafunzi wote waliweza kuendelea na masomo, tulikuwa na idadi kubwa ya waliopata Division One na Two, huku waliopata Division Three wakiwa saba tu,” alisema Bw. Machary.

Ameongeza kuwa wanapanga kuendeleza miundombinu ya shule kwa kujenga majengo mapya kutokana na mahitaji makubwa, na kwamba upatikanaji wa wawekezaji utasaidia kufikia lengo hilo.

3

“Endapo tutapata wawekezaji tutaweza kuongeza majengo na kuwafikia watoto wengi zaidi wanaohitaji msaada wa elimu,” ameongeza. Aidha, amesema shule hiyo sasa inaelekeza nguvu zaidi katika mafunzo ya ufundi stadi ili kuwawezesha wanafunzi kujiendeleza na kujitegemea wanapomaliza masomo.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa Kidato cha Nne, Afevest Kivuyo, ametaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na uhaba wa maji safi ya kunywa, chakula na vifaa vya kujifunzia hasa kwa masomo ya sayansi. “Tunaiomba serikali na wafadhili watusaidie pia kupata fursa za kufanya ‘tour’ za kielimu katika maeneo mbalimbali ili kuongeza uelewa wetu,” amesema Kivuyo.