Rais wa Zanzibar, Dk, Hussein Ali Mwinyi, ametoa msamaha kwa wafungwa 17 waliokuwa wakitumikia adhabu katika Chuo cha Mafunzo Zanzibar (Magereza), ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ikulu, katika msamaha huo, wafungwa 11 walikuwa wakitumikia adhabu katika Gereza la Unguja, huku wengine sita wakitoka Gereza la Pemba.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni utaratibu wa kawaida unaofanywa na Rais wa Zanzibar katika nyakati za maadhimisho ya kitaifa, hususan yale yenye umuhimu mkubwa wa kihistoria kwa Taifa.
Msamaha huo umetolewa kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa Rais chini ya Kifungu cha 59 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kinachompa uwezo wa kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyehukumiwa kwa kosa lolote, kubadilisha au kupunguza adhabu iliyotolewa na Mahakama.
Akieleza dhamira ya hatua hiyo, serikali imesema msamaha huo unalenga kuonesha utu, huruma na kutoa fursa ya pili kwa wafungwa waliobainika kuonesha mwenendo mzuri na nidhamu wakati wa kutumikia adhabu zao, sambamba na kuhamasisha mabadiliko chanya katika jamii.
Hatua ya Rais Dk. Mwinyi imetajwa kuwa ni sehemu ya kuenzi misingi ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, ambayo pamoja na mambo mengine yalilenga kujenga jamii yenye haki, usawa na utu kwa wananchi wote.
Maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi yanaendelea kufanyika visiwani Zanzibar, kwa shamrashamra mbalimbali, huku Serikali ikitumia fursa hiyo kutafakari mafanikio yaliyopatikana pamoja na kuweka mikakati ya kuimarisha ustawi na maendeleo ya wananchi kwa siku zijazo.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED