ZIKIWA zimebaki siku tatu Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na Madiwani kufanyika, zaidi ya makarani waongoza wapiga Kura 680 wameapishwa katika Jimbo la Mbeya vijijini kwa ajili ya kwenda kufanya kazi hiyo.
Makarani hao wameapishwa Leo wakati wa mafunzo mafunzo ya kuwaandaa kwenda kufanya kazi hiyo ikiwa ni utekelezaji wa ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo, Gideon Mapunda amewataka makarani hao kwenda kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria na kanuni za Uchaguzi ili kuepuka kuwa chanzo cha vurugu kwenye vituo vya kupigia Kura.
Amewataka kusoma Sheria na kanuni hizo na kuzielewa ili wakafanye kazi kwa weledi wakishirikiana na maofisa wengine wakiwemo mawakala wa vyama vya siasa pamoja na wengine ambao kwa mujibu wa Sheria wanaruhusiwa kuingia kwenye vituo.
"Muende mkasome katiba ya nchi, lakini ni muhimu mkawa mnafuata maelekezo yote mtakayokuwa mnapewa na Tume, msiwe chanzo cha vurugu kwenye vituo," amesema Mapunda.
Amewasisitiza kuwa na mawasiliano ya karibu na Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo na Ofisa Uchaguzi kwa ajili ya kufafanuliwa mambo ambayo watakuwa hawayaelewi ili wasiharibu kazi na kwamba wakiharibu watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED