Halmashauri ya Mji Handeni mkoani Tanga imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 531.1 kwa vikundi 127 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la serikali la kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya makundi maalum.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hundi kwa wanufaika hao mjini Handeni, Katibu Tawala wa Wilaya ya Handeni, Magreth Killo, akimwakilisha Mkuu wa Wilaya Salum Nyamwese, alisema serikali imejipanga kuhakikisha makundi hayo yanajikwamua kiuchumi na kupunguza utegemezi katika jamii.
Killo alisisitiza kuwa uaminifu na uwazi ni misingi muhimu katika utekelezaji wa miradi hiyo, akipiga marufuku tabia ya kutoa taarifa za uongo wakati wa kuomba mikopo au kukaguliwa.
“Udanganyifu unadhoofisha jitihada za serikali katika kujenga jamii yenye uadilifu. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonyesha kwa vitendo dhamira ya kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mikopo isiyo na riba, elimu ya biashara na ujasiriamali, pamoja na mafunzo ya huduma bora ili mjikwamue kiuchumi,” alisema Killo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Toba Mhina, aliwataka wanufaika wa mikopo hiyo kuhakikisha wanaitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kurejesha kwa wakati ili vikundi vingine pia vinufaike.
Naye, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Fred Mpondachuma, alisema jumla ya vikundi 244 viliwasilisha maombi ya mikopo, lakini baada ya uchambuzi wa kina vikundi 127 pekee ndivyo vilivyokidhi vigezo.
“Baadhi ya vikundi viliondolewa kwenye mpango huu kutokana na udanganyifu wa taarifa, ikiwemo kutoa taarifa za uongo kuhusu wanachama au miradi yao. Kwa mfano, kulikuwa na kikundi ambacho asilimia 80 ya wanachama wake hawakuwa wakazi wa Handeni bali wa wilaya nyingine,” alisema Mpondachuma.
Ameongeza kuwa tangu mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri hiyo imetoa mikopo ya jumla ya Sh. milioni 953.6 kwa vikundi 304, ikiwemo vikundi vya wanawake 206, vijana 74 na watu wenye ulemavu 24, huku kiasi cha Sh. milioni 511.44 sawa na asilimia 54, kikiwa kimekwisharejeshwa.
Baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru serikali kwa jitihada hizo, wakibainisha kuwa mikopo hiyo imewasaidia kuboresha biashara zao, kuongeza kipato na kubadilisha maisha yao kwa ujumla.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED