Wasimamizi wa vituo vya kupigakura watakiwa kuyapa kipaumbele makundi maalum

By Shaban Njia , Nipashe Jumapili
Published at 04:48 PM Oct 26 2025
Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Kahama mjini Sadick Juma akifungua mafunzo kwa wasimamizi wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura leo.
PICHA; SHABAN NJIA
Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Kahama mjini Sadick Juma akifungua mafunzo kwa wasimamizi wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura leo.

WASIMAMIZI wa vituo 669 vya kupigia kura katika jimbo la Kahama mjini wametakiwa kuhakikisha wanawapa kipaumbele wapigakura wanaotoka katika makundi maalum ili kuhakikisha ushiriki wa makundi hayo unakuwa wa haki na usio na usumbufu.

Pia wametakiwa kutumia lugha nzuri ya heshima na yenye staha wanapowahudumia wapiga kura wote, ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa amani, usawa na haki siku ya jumatano  Oktaba 29 mwaka huu.

Msimamizi wa uchaguzi jimbo hilo Sadick Juma ameyabainisha haya leo wakati akifungua mafunzo kwa wasimamizi wa vituo 669 na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura 1,338 yaliyolenga kuongeza uelewa kuhusu utendaji bora katika siku ya uchaguzi.

 Amesema, kila msimamizi anawajibu wa kutumia lugha nzuri yenye heshima na staha wanapowahudumia wapiga kura wote, ili kudumisha amani na kuimarisha imani ya wananchi katika mchakato wa uchaguzi, huku makundi ya wazee, wenye ulemavu, wajawazito na wanaonyonyesha wapewe kipaumbele.

 “Tunataka kuona kila mpiga kura anatendewa haki na kwa upole, lugha nzuri na huduma yenye heshima ni msingi wa uchaguzi wa kidemokrasia nasio vinginevyo”Ameongeza Juma.

 Mwenyekiti wa mafunzo hayo, Robert Japhet amesema wanaipongeza juhudi za Tume katika kuendelea kutoa mafunzo na miongozo inayolenga kuboresha upigaji kura, wakisema hatua hiyo itasaidia kuongeza uwazi, usawa na ufanisi katika uchaguzi.