JUMLA ya vibanda sita vya biashara vimeungua kwa moto huku vibanda vingine saba vikiokolewa, kufuatia hitilafu ya umeme iliyotokea katika moja ya vibanda vya biashara vilivyoko eneo la Igalilimi kata ya Kahama mjini usiku wa kuamkia leo.
Aidha moto huo ulioanza ghafla majira ya saa tatu usiku ulisababisha taharuki kubwa kwa wafanyabiashara na wakazi wa eneo hilo, baada ya kuonekana moshi ukipanda kutoka kwenye kibanda kimoja cha kuuza vifaa vya umeme, kabla ya kuenea kwa kasi katika vibanda vya jirani.
Mmoja wa shuhuda wa tukio hilo Paul Hamka amesema, amepata taarifa za kuibuka moto huo akiwa nyumbani kwake na kukimbia haraka kwenda kushirikiana na wenzake kuzima moto na kuokoa mali zilizopo kwani duka lake lilikuwa jirani na moto.
Amesema, jeshi la zima moto na uokoaji lilifika kwa wakati lakini waliishiwa maji na kulazimika kutumia bomba la maji lililokuwepo jirani ya maduka hayo lakini moto uliwazidi mpaka lilipofika gari la kuzima moto kutoka Mgodi wa Barrick Buzwagi na kuuzima.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji mkoa wa Shinyanga, ASF, Fatma Sato amesema, walipata taarifa za moto majira ya saa tatu usiku na walifika kwa wakati na kushirikiana na wananchi kuanza kuuzima moto huo.
Amesema, moto ulikuwa mkubwa kutokana na baadhi ya maduka ya biashara kuwa na magodoro, vitambaa, nguo na maboksi hatua iliyowafanya watu wa mgodi wa Barrick Buzwagi kuongeza nguvu na kufanikisha kuuzima ndani ya nusu saa.
Aidha amesema,hakuna kifo wala majeruhi yeyote aliyepatikana kwani wananchi walichukua tahadhari wakati wa zoezi la uzimaji wa moto na chanzo chake ni hitilafu ya umeme iliyotokea katika moja ya duka.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amewataka wafanyabiashara wote mkoani humo kuhakikisha wanaweka vitambuzi vya moto katika maeneo yao ya biashara, ikiwa ni hatua ya kujikinga na majanga ya moto yanayoweza kusababisha hasara kubwa za mali na kuhatarisha maisha ya watu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED