Mahakama yamuhukumu kifungo cha nje baba aliyeua mwanaye

By Grace Gurisha , Nipashe Jumapili
Published at 01:15 PM May 11 2025
news
mtandao
Alama ya hukumu

MAHAKAMA Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya imemuhukumu, Ramadhani Mwakilasa kifungo cha nje baada ya kukutwa na hatia ya kumuua mtoto wake wake wa pekee, Chloe Ramadhani (4) bila kukusudia wakati akimuadhibu kwa kujisaidia kwenye nguo.

Aidha, Mahakama hiyo imesema kitendo cha mshtakiwa kurudi nyumbani kutoka kazini kama mwanaume na baba wa mtoto, na kuanza kumsafisha mtoto wake kutokana na uchafu wake, kinaonesha kuwa mshtakiwa alikuwa na mapenzi na kujali mwanaye. 

Marehemu alikwenda kumtembelea baba yake ambaye alikuwa akiishi na mke wake (mama wa kambo wa marehemu) katika eneo la Teku Viwandani ndani ya Wilaya na Mkoa wa Mbeya. Mama mzazi wa ambaye anaishi Dar es Salaam alimruhusu mtoto kwenda kumtembelea baba yake. 

Katika kipindi cha kuishi pamoja, mshtakiwa alikuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na mama mzazi wa marehemu akilalamika kuwa marehemu alikuwa akijikojolea na kujisadia mwenyewe, na alikuwa akimwadhibu kwa tabia hiyo. 

Novemba 25, 2024, wakati mshtakiwa akijiandaa kurudi nyumbani kutoka kazini, mshtakiwa alipokea simu kutoka kwa mke wake (mama wa kambo) aliyemjulisha kuwa marehemu amejisadia tena. 

Alipofika nyumbani alimkuta marehemu akiwa amevaa nguo zilezile alizojichafua nazo, alianza kumpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake kama njia ya kumwadhibu, kisha akamwogesha kwenye beseni la kuogea, alipomwambia asimame hakuweza. 

Alipokwenda kuchukua taulo, aliporudi alimkuta marehemu akiwa amelala kwenye beseni akiwa hajitambui.Alijaribu kumwamsha lakini hakuitika, alimchukua na kumpeleka kwa babu yake, ambaye aligundua kuwa tayari amefariki dunia. 

Mshtakiwa alikiri mbele ya polisi na mbele ya mlinzi wa amani kuwa alisababisha kifo cha mtoto wake wakati akimwadhibu, na kwamba ilibainika kuwa chanzo cha kifo cha marehemu kilikuwa ni majeraha ya kichwani. 

Mshtakiwa alihukumiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia (Manslaughter) kinyume na Kifungu cha 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, ambacho kina adhabu ya hadi kifungo cha maisha jela. 

Jaji Victoria Nongwa alisema katika mazingira ya kesi hiyo, na kwa kuzingatia mwongozo wa utoaji wa adhabu, uzito wa kosa hilo umewekwa katika kiwango cha chini (low level) kwa kuwa kifo kilisababishwa na adhabu ya kawaida aliyopewa mtoto na mzazi wake. 

"Nimezingatia hoja za kupunguza adhabu zilizowasilishwa na wakili wa utetezi kama zilivyoelezwa hapo juu, pamoja na ukweli kuwa mshtakiwa amekuwa akishirikiana kikamilifu tangu alipokamatwa, na leo hii amekiri kosa," 

"Mshtakiwa amekuwa akilia muda wote wa kusikilizwa kwa kesi na alifanikiwa kueleza jinsi alivyoguswa na kujuta kwa yaliyomtokea mtoto wake wa pekee. Kitendo cha kurudi nyumbani kutoka kazini kama baba na kuanza kumsafisha mtoto wake kutokana na uchafu wake, kinaonesha kuwa mshtakiwa alikuwa na mapenzi na kujali kwa mtoto wake," alisema Jaji Nongwa 

Jaji Nongwa alisema kwa sababu  mshtakiwa amekiri kosa, anastahili kupunguziwa adhabu halisi ambayo angepewa kama kesi ingesikilizwa hadi mwisho na kupatikana na hatia. 

Kutokana na hoja za upande wa utetezi, Jaji Ngongwa alisema inaonesha kuwa mshtakiwa amekaa rumande kwa muda wa miezi sita, muda huo unaotosha kwake kujifunza. 

"Kwa mazingira haya, mahakama hii inamhukumu mshtakiwa kwa kuachiwa kwa masharti kwa muda wa miezi  12. Haki ya kukata rufaa iko wazi kwa ambae hajaridhika,"alisema Jaji Nongwa.