SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) mkoa wa Morogoro limewataka wapangaji wa jengo la Lottos ambalo wanamiliki kwa ubia na mwekezaji Sameer Ismail Lotto kuondoka kwa hiyari ili kupisha matengenezo ya kukamilisha jengo hilo baada ya mwekezaji huyo kudaiwa kusuasua kwa muda mrefu kulikamilisha.
Meneja wa NHC Mkoa wa Morogoro,Lwitiko Ndigha Alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari waliofika ofisini kwake baada ya kupokea malalamiko ya baadhi ya wapangaji walioomba majina yao kuhifadhiwa wa jengo hilo kudai kupewa notisi ya siku saba na NHC kuondoka na kupisha matengezo.Meneja huyo wa NHC mkoa wa Morogoro alikiri wamelazimika kutoa notisi hiyo baada ya mwekezaji kushindwa kufanya hivyo licha ya kukubali kwenye vikao mbalimbali.Akakiri ni kweli wana ubia na Lotto lakini kwa muda mrefu amekuwa akijenga jengo hilo bila kukamilika hivyo walifikia maamuzi hayo ya kuondoa wapangaji ili Shirika likamilishe Ujenzi na kwa ubora.
Akasema baadhi ya wapangaji wamepokea na kusaini kukubali kuondoka ila wachache hawajapokea na kwamba watakaosaini kukubali kuondoka kwa hiyari ndio watapewa kipaumbele cha kupanga tena jengo hilo mara baada ya kukamilika.
Timu ya waandishi wa habari ikamtafuta mwekezaji wa jengo hilo Sameer Ismail(Lottos)kuzungumzia hali hiyo ambapo alisema hataki kuzungumzia kuhusu wapangaji kupewa notisi na kutakiwa kuondoka kwani suala hilo lipo mahakamani na wanasubiri lianze kusikilizwa ingawa akawasihi wapangaji hao kuwa watulivu wakati hilo likifanyiwa kazi.
"Mwaka 2006/2007 niliingia mkataba na Shirika la Nyumba na kuanza ujenzi, ambapo walinitaka kujenga jengo la ghorofa sita lakini niliwaeleza uwezo wangu ni kujenga jengo la ghorofa tatu, na kuna namna nyingi tumepita Katika Ujenzi, kwani awali walikubali wangeniandika kwenye nyaraka ili nipewe mikopo kulimalizia, lakini hilo likashindikana" alisema Lotto, Mbunge wa zamani wa Morogoro Kusini Mashariki.
"Toka wakati huo sijawahi kuwa na utulivu kwenye huu Ujenzi, nimehangaika sana, na wakaguzi waliletwa na NHC na nikawaridhia kuja kukagua ubora wa jengo hili na wakaridhia liko sawa tuendelee na Ujenzi ila liishie hapa hapa nilipokuwa nimefikia" alisema Lotto.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED