SERIKALI imeanza kusimamia ujenzi wa barabara ya kutoka Banana kwenda Kitunda, Kivule Msongola, Majohe na Njia Nne, kwa kiwango cha lami ambazo zilikuwa kero kwa wakazi wa maeneo hayo kwa muda mrefu
Barabara hizo zimeanza kukarabatiwa kuanzia Januari 15, mwaka huu, hadi kufika Mei 30, mwakani, zinatarajiwa kukamilika, zitakuwa za kiwango cha lami, huku gharama zake ni sh. bilioni 30.368 na wakandarasi wanaendelea na ujenzi huo.
Akizungumza na mwandishi wa habari wa gazeti hili, baada ya kutembelea na kukagua barabara hizo zilizoathiriwa na mvua, Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Geofrey Mkinga, amesema barabara ya Banana hadi Msongola ina urefu wa kilomita 13.18 na Kivule hadi Majohe njia nne ni 2.79.
“Mradi wetu wa DMDP awamu ya pili imekwishaanza, wakandarasi wapo wanaendelea na kazi za awali na watu wa vipimo wapo, barabara ya Kivule-Majoe njia nne inapita katika Hospitali mpya ya Wilaya ya Ilala, ambayo itakuwa na umuhimu mkubwa kwa wananchi kusafiri kwausalama zaidi.
“Tunawaomba wakazi wa maeneo hayo, kuendelea kuwa na imani na Serikali kwa kuwa, TARURA ipo kwa kusikiliza wananchi na kuendelea kutekeleza changamoto zote zitakazotokea za barabara,” amsema.
MAJI KUJAA BARABARANI
Akizungumzia changamoto alizokutana nazo katika ziara hiyo, Meneja huyo, amesema chanzo kikubwa ni baadhi ya watu kuziba njia za maji za asili na kusababisha maji kubaki barabarani kukosa mwelekeo mzuri.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mkinga, barabara zinapokuwa zinakarabatiwa hususani za udongo basi, zinashindwa kuhimili maji yanapotokea na kutengeneza mashimo.
“Tumeweza kutembelea barabara ya Banana hadi Msongola, ambayo ina mkandarasi, tumeona changamoto zilizopo kuna maeneo ya Kizuiani na Matembele ya Kwanza yana changamoto kubwa sana ya kuwapo na mashimo makubwa ambayo mvua inaponyesha magari madogo yanashindwa kupita na hata ya abilia pia kualibiku na kupelekea wenye magari kuamua kuyaota magari yao kutokana na ubovu wa barabara hiyo.
“Nitoe rai kwa wananchi kuheshimu njia za maji kwa kuwa, wakifanya hivyo watasababisha uwepo wa mafuriko katika barabara na kuleta athari za kuharibu barabara na magonjwa ya vipindupindu katika makazi wanayoishi,” amesema.
NINI CHA KUFANYA
Mhandisi Mkinga alisema baada ya kubaini changamoto hizo, alimwelekeza mkandarasi kufanya matengenezo ya barabara hiyo ya Banana hadi Msongola, kuweka kifusi chenye mawe maeneo yenye mashimo makubwa.
Pia, alimuagiza Meneja wa TARURA Wilaya ya Ilala, Mhandisi John Cheche, wale wote walioziba na kujenga katika njia za maji, kuzifungua mara moja kwa kuwa, maji yanajaa barabarani na kukosa sehemu ya kwenda.
“Mpango uliopo hivi sasa ni kujenga madaraja makubwa ambayo yatapitisha maji kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi, sehemu ya Viwege madaraja yatawekwa, hivyo wakazi wa maeneo hayo waendelea kuvumilia,” amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Ilala, Mhandisi Cheche, ambaye ni msimamizi wa mradi wa DMDP awamu ya pili, alisema atasimamia maelekezo aliyopewa, huku akiwasihi wananchi kulinda njia za maji.
“Sisi tutaendelea kumsisitiza mkandarasi wa barabara ya Banana hadi Msongola, kuendelea kukarabati na kuhakikisha barabara hiyo inazibwa mashimo kwa kuweka mawe, wananchi wapite vizuri.
Mkazi wa Kivule, Amina Hassan, amewashukuru TARURA kwa kuanza kuweka vipimo vya kukarabati barabara hiyo itakayotarajiwa kujengwa katika kiwango cha lami amesema endapo barabara hiyo ikikamilika itakuwa imewaondolea adha ya kutumia gharam kubwa ya nauli, amesema kwa sasa wananchi wa Kitunda na vitongoji vyake wanatumia nauli kubwa jambo ambalo linawapotezea kipato chao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED