WAKULIMA wa mazao ya chakula na biashara Kanda ya Ziwa, wameitwa kuchangamkia fursa ya mikopo ya zana za kilimo, zinazotolewa na taasisi za kifedha kwa kushirikiana na kampuni ya Agricom, ili kuwawezesha kulima na kupata mavuno ya kutosha.
Meneja wa kampuni hiyo Kanda ya Ziwa, Christina Mabula, ameyabainisha hayo, wakati akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari namna wanavyoshirikiana na taasisi za kifedha katika kuwawezesha wakulima wa mazao ya chakula na biashara katika kukuza sekta ya kilimo.
Amesema, wana zana za kilimo zenye uwezo wa kulima maeneo makubwa kwa muda mfupi na zitawasaidia wakulima kuondokana na kutumia jembe la mkono, ambalo huchukua muda mrefu shambani.
“Sisi tunataka mkulima aondokane na kutumia jembe la mkono, ng’ombe au punda shambani kwa sababu zana za kilimo za kisasa na zenye uwezo tunazo na mkulima mwenye uwezo atanunua na wale wanaotaka mkopo tunawaunganisha na taasisi za kifedha tulizoingia nazo ubia,” ameongeza.
Mabula amesema, wamekuwa wakifanya kazi na bodi za kilimo katika kukuza sekta hiyo na mwaka 2023, Bodi ya pamba ilichukua matrekta 400 kati yake TCB ilichukua trekta 3,000 na TCA 100 na kusababisha kuongezeka kwa kilimo cha pamba nchini.
Mkulima wa Chama cha Msingi Uyogo, William Masanja, amekiri kutumia zana duni hasa ya jembe la kuvutwa na ng’ombe wakati wa kilimo na kuchukua muda mrefu kumalima shamba.
Mtoa huduma baada ya mauzo, Mhandisi Fredy Emmanuel, amesema wanafundisha kuanzia ngazi za vijiji mpaka taifa ambao wanawafikia wakulima na kufundisha namna ya kutumia zana za kilimo za kisasa wakati wa kilimo na utengenezaji pale chombo kinapoharibika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED