MAKADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliotia nia kuwania ubunge na uwakilishi katika majimbo na makundi maalum, wamewekwa roho juu.
Hatua hiyo ni baada ya chama hicho tawala kusogeza mbele uteuzi wa wanachama watatu wa uwakilishi na ubunge katika kila jimbo Tanzania Bara na Zanzibar kwa ajili ya kupigiwa kura na hatimaye kufanya uteuzi wa mwisho wa watakaopeperusha bendera ya chama katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Awali, chama hicho kilitarajia kufanya vikao vya ngazi ya juu jana na leo na kutoa orodha hiyo lakini sasa, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana. Kutokana na mabadiliko hayo, kinatarajia kufanyika Julai 28, mwaka huu.
Wakati hali ikiwa hivyo, CCM imetaja sababu ya kusogeza mbele kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC - NEC) kuwa lengo ni kujipa muda wa kutosha kuwachambua kwa umakini watiania na kuwatendea haki.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Amos Makalla, alisema hayo jana jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari, akisisitiza kuwa idadi ya watiania waliojitokeza ni zaidi ya 30,000, hivyo kunahitajika muda wa kutosha ili kuwachambua kwa umakini.
Makalla alisema kutokana na mabadiliko hayo, wanatarajia kufanya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kitakachotanguliwa na kikao cha Kamati Kuu Julai 26, mwaka huu, jijini hapa.
“Wabunge, madiwani watiania wote ni wengi. Kazi ni kubwa na tunataka tuifanye kwa umakini na utulivu, hivyo, uteuzi wa mwisho utafanyika Julai 28, mwaka huu,” alisema Makalla.
Alisema ni muhimu CCM ikazingatia umakini katika mchakato huo kwa kuwa wao ndiyo waliotoa ratiba, na mchakato huo ni wa ndani ya chama.
“Ninyi ni mashahidi, nafasi za madiwani pekee zina zaidi ya watu 27,000 na ubunge zaidi ya watu 10,000. Tunapitia CV (wasifu) za (wa) watu wote hao. Hii ni kazi kubwa inayohitaji uchambuzi wa kina,” alisema.
Makalla alisema CCM iliahidi kutoa ilani bora kuliko chama chochote na itasimamisha wagombea bora, hivyo chama hakijafungwa katika muda wowote wa nje bali kinafuata taratibu zake.
Alisisitiza kwamba mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM unaendelea vizuri na maandalizi ya kikao cha mwisho cha uteuzi yanaendelea kabla ya wagombea kwenda katika kura za maoni.
“Leo (jana), wengi walitarajia kwamba Kamati Kuu ingeanza kikao chake na kufanya uteuzi wa mwisho, lakini tumeamua tukutane Julai 26. Wagombea wanapaswa kuwa watulivu wakati mchakato unaendelea,” alisema.
Makalla alisema kazi ya uchambuzi ni kubwa, hivyo chama kinahitaji muda wa kutosha kuhakikisha haki inatendeka kwa wagombea wote.
“Uteuzi wa mwisho utafanyika Julai 28. Wagombea watulie hadi hapo. Baada ya hapo, chama kitatoa ratiba ya kwenda kura za maoni.
“Chama ni makini na kina uzoefu, na hakutakuwa na mtu aliyeenguliwa hadi Julai 28 ambayo itakuwa ni tarehe rasmi ya kutangaza uteuzi wa mwisho,” alisema.
Kuhusu masuala ya mashinikizo, Makalla alitoa wito kwa wanachama kufuata taratibu za chama, akisisitiza kuwa kuna vikao vinavyopaswa kuamua kwa mujibu wa Katiba ya CCM.
“Tuliposema wasiende kuchukua fomu na matarumbeta au maandamano, tulimaanisha. Sasa kila mmoja angekuja na watu wake, mnaamua nani alikuja na matarumbeta mengi? Hivyo, wawe watulivu. Chama kitafanya uteuzi na kuwapa taarifa rasmi,” aliongeza.
Alifafanua kuwa hakuna mtu aliyekatwa wala kufyekwa, na kwamba, taarifa rasmi ya uteuzi wa wagombea itatolewa Julai 28.
Kuhusu madiwani wa viti maalum, alisema kuwa majina tayari yameridhiwa na yamepelekwa kwa ajili ya kura za maoni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED