RIPOTI MAALUM; Wimbi watu kujiua lashtua wataalam

By Waandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 01:07 PM Jul 20 2025
Mtafiti Mwandamizi katika Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), Dk. Donat Shamba
Picha: Mpigapicha Wetu
Mtafiti Mwandamizi katika Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), Dk. Donat Shamba

NI mshtuko katika jamii. Hiyo ni kutokana na ongezeko la matukio ya watu kujiua ambalo sasa linashika kasi huku sababu mbalimbali zikitajwa.

Sababu kubwa zinazotajwa kuonmgezeka kwa matukio hayo ni wivu wa kimapenzi, hali ngumu ya maisha, maradhi ya muda mrefu na sugu, migogoro ndani ya familia na kukosa ajira au shughuli za kufanya licha ya kuwa na elimu. 

Wataalam wanasema ongezeko hilo pia linachangiwa kukosekana kwa huduma madhubuti za afya ya akili, uhaba wa wataalamu na unyanyapaa.

Pia wanataja miongoni mwa dalili za mtu mwenye tatizo la afya ya akili kuwa ni kujikataa na kujinyanyapaa, kukwepa kuonana na watu kunakosababishwa na msongo wa mawazo (stress). Nyingine ni mtu kufanya vitu kupita kiasi, ikiwamo kazi au pombe.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Mtafiti Mwandamizi katika Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), Dk. Donat Shamba, anasema mtu anaweza kufanya vitu kupita kiasi kuanzia saa 2:00 usiku hadi saa 12:00 asubuhi na mwingine hataki kuonana na watu na kwenye shughuli zozote kama harusi haendi.

Dk. Shamba anasema tatizo la afya ya akili (isipokuwa lililotokana na matumizi ya dawa za kulevya) ni ugonjwa unaoweza kumpata mtu yeyote, kulingana na ubongo wake unavyoweza kutafsiri taarifa hasa mbaya.

Anasema pamoja na ukweli huo, utamaduni uliojengeka katika jamii unaifanya familia ya mgonjwa kudhani mtu akipata shida ya akili, amelogwa na tiba ni kwa mganga wa jadi au kwenye maombi kanisani au kwa shekhe.

“Ndiyo sababu mtu anaweza kupata tatizo leo akaanza kwenda kwa mganga au kanisani kuombewa badala ya kwenda hospitalini. Na hii ni moja ya changamoto inayokuza tatizo. Lakini pia uhamasishaji wa upatikanaji wa huduma hizi na wapi ziliko pia ni mdogo,” anasema.

Dk. Shamba anasema jamii inavyolichukulia tatizo hilo ni tofauti na magonjwa mengine kama Malaria, ambako mtu akiona dalili anawahi kituo cha afya kupima na kupata dawa. Na hili linasababisha mtu anafika hospitali kwa kuchelewa sana. Anakuja ameanza kudhuru watu au kujifungia ndani na kujidhuru mwenyewe au anataka kujiua,” anasema.

Kingine, anasema  ni uelewa na matarajio ya familia kwa mgonjwa kabla hajaanza kuugua, jambo linalomkwamisha mtu kusema pale wanapokumbwa na changamoto za maisha.

“Mtu akipata hii shida kuna watu wanasema anajifanyisha. Wengine  wanasema huyu atakuwa amekuwa kichaa au chizi. Hii  inasababisha aonekane hana mchango wowote kwenye jamii na kumkataa na kusema huyu ndio basi tena na familia au jamii haiweki jitihada zozote kumsaidia,” anasema.

Kadhalika anasema utamaduni huo unamuathiri zaidi mgonjwa kwa kuona hathaminiki na hivyo kujitenga na kuzidi kukuza ugonjwa.

“Tatizo hili haliangalii kipato cha familia, linawakuta watu wa hali zote, masikini na matajiri…kwa namna  tulivyoona kwenye utafiti, wagonjwa wanaotoka familia tajiri wengi wanachangamoto kubwa zaidi, kwa sababu familia hazitaki zionekane kwamba wana mtu mwenye changamoto ya afya akili, watu wanataka kujificha kuonesha wako sawa,” anasema.

Dk. Shamba anasema kwenye kaya masikini, wagonjwa wengi wanaonekana wamelogwa na wanaanza dozi na kukatisha kwa kupelekwa kwa waganga au kwenye maombi. Pia anasema wataalamu wa afya ya akili nchini ni wachache ikilinganishwa na idadi ya watu.

Anatoa mfano kwamba katika bima nyingi za afya, ugonjwa wa afya ya akili haujapewa kipaumbele, hali inayokwamisha uelewa wa jamii kuhusu huduma hizo kupatikana hospitali.

Kuhusu watu wanaokumbwa na changamoto hiyo, Dk. Shamba anasema wanatoka katika familia za vipato vikubwa, vya kati na vidogo, unyanyapaa ukiwakabili wote bila kujali hali ya uchumi au elimu ya familia.

Anasema mgonjwa na watu wake wa karibu, wanaweza kubaini dalili hizo na kuweza kuchukua hatua mapema.

Ili kukabili tatizo hilo, anasema wadau wa afya wanapaswa kuweka mikakati ya kujenga uelewa wa umma kuhusu dalili na upatikanaji wa huduma.

“Mtu anaweza kujitambua kama ana hii shida, kikubwa ni kuboresha njia za kujikinga kwa kujenga uelewa kwa jamii. Kwa kuanza kutoa elimu kuanzia shule za  singi, ili watoto na vijana wajue dalili na wajue nini wafanye wanapokumbwa na changamoto. Kuna watoto pia wanajiua,” anasema.

NINI KIFANYIKE

Dk. Shamba anasema watu waambiwe kuna hili tatizo na ni la kawaida, huweza kumpata binadamu yeyote. “Tatizo ni dhana iliyojengeka kwamba ukipata changamoto ya afya ya akili unaonekana umelogwa. Ni tatizo linaloweza kukupata wakati unazaliwa (pathological).

“Vingine ni namna tulivyoumbwa na utendaji wa ubongo pale unapopata jambo fulani. Huduma ziboreshwe na kuwe na namna ya utambuzi mapema, maana mara nyingi wagonjwa wanabainika kwa kuchelewa,” anashauri.

Dk. Shamba pia anashauri kuongezwa kwa wataalamu wa changamoto ya afya ambao watatoa huduma kuanzia ngazi ya Kituo cha Afya, Hospitali za Wilaya, za Rufani za Mikoa na Kanda hadi ya Taifa, Muhimbili.

Anasema sambamba na wataalamu, miundombinu ya kutoa huduma hizo ijengwe kuanzia vituo vya afya na hospitali za ngazi zote, ili kuweka mazingira ya wananchi kupata huduma hizo kwa uhakika.

UTAFITI

Dk. Shamba anasema utafiti uliohusisha nchi zenye kipato cha juu, kati na masikini, umebaini kwamba, ili kukabiliana na uhaba wa watalaamu, watu waliopona changamoto hizo (peer support), wakijengewa uwezo, wanaweza kuwasaidia wagonjwa katika ngazi ya jamii.

“Lengo la kutimia mtu ambaye amepata changamoto ya afya ya akili akapona, anakuja kuwasaidia wengine ili kwenda nao katika hatua ya kupona. Mfano mtu anatoa ushuhuda wake alivyopona msongo wa mawazo, aliwezaje kutumia dawa, yule anayeumwa sasa hivi akielezewa hizo changamoto anapata matumaini kwamba huyu alikuwa na hali kama yangu, lakini mwisho wa siku akapona,” anasema.

Anasema utafiti umethibitika kuleta matokeo chanya kwa nchi zote, na kwamba wenye changamoto ya afya ya akili, wanakabiliwa na matatizo yanayofanana, ukiwamo unyanyapaa binafsi na ule unaofanywa na jamii.

“Kwa kutumia ‘peer support’, kunamfanya mgonjwa aone bado ana umuhimu, anakuwa na matumaini, anajiona ana muhimu. Matokeo ya utafiti wetu yamethibitisha mabadiliko makubwa kwa watu hawa kujiona wa maana na kunakuwa na ujumuishaji ndani ya familia,” anasema.

Pia anasema kundi hilo likijengewa uwezo, linaunganisha wagonjwa na hospitali; na kuwapa wagonjwa matumaini ya kupona baada kutumia dawa.

Watoa huduma hao hutumia uzoefu wao wa maisha, kufungua mioyo yao kwa namna chanya, kupanua mitandao yao ya kijamii, na kuendeleza matumaini, uwezeshaji na uwezo wa kujiamini.

Utafiti huo wa kimataifa uliomhusisha Dk. Shamba na wanasayansi wengine kutoka Ujerumani, Israel, India, Uganda na Tanzania, ambao umechapishwa katika jarida la British Journal of Psychiatry, mwezi huu, unaonesha kwamba msaada wa ‘peer support’, una matokeo makubwa ya haraka kwa wagonjwa.

Nchi zilizohusika kwenye utafiti huo ni Ujerumani, Israel, India, Uganda na Tanzania, ukihusisha wagonjwa 615 wakiwamo 305 waliopokea msaada wa watu waliopona tatizo hilo.

“Kujitenga kijamii ni moja ya sababu kuu za kuzorota kwa afya ya akili, na kwamba uwezeshaji na matumaini ni muhimu katika mchakato wa kupona, msaada huu unapendekezwa kama sehemu madhubuti ya huduma za afya ya akili, badala ya kuzingatia tiba za kawaida za kitabibu pekee,” inaonesha sehemu ya matokeo hayo.

Matokeo ya utafiti huo yameonesha athari chanya katika ujumuishaji wa kijamii, uwezeshaji, na matumaini kwa watu wenye matatizo makubwa ya afya ya akili katika mazingira mbalimbali kwenye nchi hizo.

“Kwa kuwa kujitenga kijamii ni kichocheo kikuu cha matatizo ya afya ya akili, na uwezeshaji pamoja na matumaini ni vitu muhimu katika uponyaji, msaada wa wenzake unaweza kupendekezwa kama sehemu madhubuti ya huduma ya afya ya akili.”

Wanasayansi hao wanapendekeza mabadiliko katika mifumo ya afya ya akili duniani, kutoka ya tiba ya dawa na kudhibiti dalili pekee, kuelekea njia jumuishi inayojikita kwenye uhusiano wa kibinadamu na uzoefu wa pamoja.

“Jaribio letu linatoa ushahidi thabiti kuwa waliopona, wanaweza kuwa sehemu muhimu ya huduma ya afya ya akili inayolenga uponyaji katika mazingira mbalimbali,” wanasema.