Miradi ya kukabiliana na mabadiliko tabianchi yaongeza uzalishaji mazao

By Beatrice Shayo , Nipashe Jumapili
Published at 02:02 PM Jul 20 2025
Data izinazokusanywa kuhusu mabadiliko ya tabianchi zinaweza kusaidia kutoa maamuzi kuhusu kilimo, yameathiri zaidi wakulima. Hapa kama inavyoonekana pichani nchini Niger
Picha: UN
Data izinazokusanywa kuhusu mabadiliko ya tabianchi zinaweza kusaidia kutoa maamuzi kuhusu kilimo, yameathiri zaidi wakulima. Hapa kama inavyoonekana pichani nchini Niger

MIRADI ya kilimo inayozingatia mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi imetajwa kuchangia kuimarisha kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali na kuinua sekta hiyo katika maeneo mengi nchini.

Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la SNV Tanzania, Jeen Kootsra, aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mwongozo wa ufundishaji kilimo himilivu, mradi wa Craft kwa wakulima unaozingatia hali halisi ya mazingira katika mifumo ya kilimo na chakula kwa Tanzania, Uganda na Kenya kwa kushirikiana na sekta binafsi.

"Wazo la Mradi wa Craft ni kujenga uvumilivu wa hali ya hewa katika mifumo ya kilimo cha chakula kwa nchi hizi tatu kwa kushirikiana na sekta binafsi," alisema.

Kootsra alisema wakulima wa nchini wanapaswa kujengewa uwezo ili kutambua namna bora ya kufanya kilimo himilivu kwa kuzingatia mabadiliko ya tabia nchi lengo kuongeza uzalishaji na kipato.

Akizungumzia mradi huo, Ofisa Tathimini na Ufuatiliaji Mradi wa SNV Tanzania, Sophia Kessy, alisema wamekuwa wakitekeleza kwa kushirikiana na kampuni za wajasiliamali wa kati na wadogo na vyama vya wakulima wadogo ili kuwafikia wakulima hao.

Alisema mwongozo huo uliozinduliwa utatumika kutoa mafunzo na kutumika na wadau ambao wako katika sekta ya kilimo, lengo ni kuwafikia wakulima popote waliko katika mikoa yao.

"Mwongozo huu unambinu zote za kufanya kilimo himilivu na teknolojia ili kumfanya mkulima mdogo kuongeza uzalishaji, lakini pia kuongeza kipato. Tumekuwa tukiwafikia wakulima wadogo kwa kuwapa mafunzo na mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema.

Mtafiti kiongozi wa zao la viazi mvuringo, kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Kituo cha Uyole, Owekisha Kwigizile, alisema kwa kutumia kilimo bora kinachotumia teknolojia na kuzingatia mabadiliko ya tabia ni kichocheo cha ungezeko la chakula nchini.

"Sisi kama TARI tawi la Uyole tumetekeleza miongozo inayotutaka kusaidia wakulima kujifunza namna ya bora ya kulima na kuwa na kilimo chenye tija kwa maslahi yao binafsi, lakini kwa maslahi ya taifa kwa ujumla," alisema.

Mnufaika wa mafunzo yanayotolea na SNV ambaye ni  Mratibu wa Miradi kutoka EA Foods Limited, Hance Melcheor, amelipongeza shirika hilo na kuomba kuendelea kuwasaidia na wakulima wengine kupata mafunzo hayo ili waweze kulima kwa tija.

Alisema pembejeo zimewasaidia kuimarisha kilimo na kuongeza kiwango cha mazao kutoka tani nne hadi tani nane kwa ekari.