DRC hali sasa shwari

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 05:26 PM Jul 20 2025
news
Picha Mtandao
Mjumbe maalum wa Rais wa DRC Sumbu Mambu kulia, na katibu wa kudumu wa M23 Benjamin Mbonimpa wakisamiliana kwa mikono baada ya kusaini makubaliano ya amani huko Doha, Qatar.

HALI ya vita na kiusalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inatazamiwa kurudi kuwa shwari baada ya taifa hilo na kundi la waasi wa M23 kutia saini ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

Ilielezwa kuwa pande hizo mbili zilitia saini juzi kwenye tamko la kanuni ambazo masharti yake ni pamoja na usitishaji wa kudumu wa mapigano, baada ya miezi mitatu ya mazungumzo nchini Qatar.

Hatua huyo inafuatia makubaliano tofauti ya amani kati ya serikali ya Kongo na Rwanda yaliyotiwa saini mjini Washington mwezi uliopita.

DRC ikiwa ni miongoni mwa mataifa yenye utajiri wa maliasili, haswa madini yenye faida kubwa, iliingia kwenye mzozo wa vita kwa zaidi ya miongo mitatu, na kusababisha janga la kibinadamu na kulazimisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao.

Katika makubaliano hayo pande zinazozozana zilikubali kuheshimu dhamira yao ya usitishaji vita wa kudumu, ikiwa ni pamoja na kujiepusha na propaganda za chuki, na jaribio lolote la kunyakua maeneo mapya kwa nguvu.

Makubaliano hayo yanajumuisha ramani ya njia ya kurejesha mamlaka ya serikali mashariki mwa DRC, na makubaliano ya pande hizo mbili kufungua mazungumzo ya moja kwa moja kuelekea makubaliano ya amani ya kina.

Katika hatua nyingine, Umoja wa Afrika (AU) umeyapongeza makubaliano hayo mapya ukisema kuwa ni maendeleo makubwa na kwamba: “Hii... inaashiria hatua kubwa katika juhudi zinazoendelea za kufikia amani ya kudumu, usalama na utulivu mashariki mwa DRC na eneo pana la Maziwa Makuu.”

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Mahmoud Youssouf alikaribisha hatua hii muhimu na kupongeza juhudi zote zinazolenga kuendeleza amani, utulivu na maridhiano katika eneo hilo.

Pia alisema anathamini jukumu la kujenga na la kuunga mkono lililofanywa na Marekani na Dola la Qatar katika kuwezesha mazungumzo na makubaliano ambayo yalisababisha maendeleo hayo.

Aliongeza kuwa hatua hiyo inaashiria ufanisi wa juhudi zinazoendelea za kufikia amani ya kudumu, usalama, na utulivu mashariki mwa Kongo na katika eneo zima la Maziwa Makuu.

Pande hizo mbili zilisema makubaliano hayo mapya yanaambatana na ya Washington, ambayo Rais wa Marekani Donald Trump wakati huo aliyataja kuwa ni mwanzo wa enzi mpya ya matumaini na fursa kwa eneo hilo.

Msemaji wa serikali ya Kongo Patrick Muyaya alisema makubaliano hayo yamezingatia kile kinachojulikana kama mistari nyekundu ya Kongo, ikiwemo kujiondoa bila masharti kwa M23 katika maeneo yaliyokamatwa na kisha kupelekwa kwa vyombo vyao vya dola wakiwemo wanajeshi.

Pande hizo mbili zilikubaliana kutekeleza masharti ya makubaliano hayo ifikapo Julai 29, na kuanza mazungumzo kuelekea makubaliano halisi ifikapo Agosti 8, mwaka huu.

Rais wa Rwanda Paul Kagame na Rais wa Kongo Felix Tshisekedi wanatarajiwa kukutana katika miezi ijayo ili kuutia nguvu mkataba wa amani wa Washington, ambao masharti yake bado hayajatekelezwa.