Msako mkali waliomchokoza Balozi Sirro

By Augusta Njoji , Nipashe Jumapili
Published at 02:46 PM Jul 20 2025
Balozi Simon Sirro
Picha: Mtandao
Balozi Simon Sirro

MKUU wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amesema kwa sasa kuna oparesheni zinafanywa na polisi kwenye wilaya zote za mkoa huo kuwasaka waliofanya uhalifu wa utekaji wa gari katika tukio lililotokea wilayani Kibondo hivi karibuni.

Katika tukio hilo, wahalifu hao waliteka basi la abiria na kuwapora vitu mbalimbali vikiwamo fedha, simu na nguo.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dodoma kupitia mpango wa Idara ya Habari (MAELEZO) wa kueleza mafanikio ya serikali ya awamu ya sita, Sirro ambaye pia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kwenda kwenye mkoa huo ambao unahitaji mtu wa aina yake.

“Mkoa wa Kigoma kwa ujumla umekuwa tulivu licha ya kuwa na matukio machache ya uhalifu. Jeshi  la Polisi Mkoa wa Kigoma kupitia vitengo vyake  limeendelea na majukumu yake kuhakikisha unakuwa shwari. Ukiangalia  takwimu, kuna upungufu mkubwa wa unyang’anyi wa kutumia silaha,”alisema.

“Matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha ni yale yanayotokea mara moja moja kwa kuvizia na yanapotokea, vyombo vyetu kwa kushirikiana na wananchi vimekuwa vinawapata watuhumiwa.

“Kama mnavyokumbuka hivi karibuni walinibipu na nikasema nitawapigia. Kwa  taarifa nilizo nazo, oparesheni zinaendelea na askari wetu wako wengi na sasa wako maeneo yote. Si  eneo la Kibondo tu. wako mkoa mzima. Ni  operesheni kuhakikisha hawa waliofanya tukio hili wanakamatwa na kupelekwa mahakamani,” alisema.

Pia alisema makosa makubwa ya jinai yaliyoripotiwa kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Juni,  2024 yalikuwa 1,653 kulinganisha na kipindi cha Julai 2024 hadi Juni, mwaka huu ambayo ylikuwa ni 1,531.

Balozi Sirro alisema idadi ya makosa dhidi  ya maadili ya jamii kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Juni, 2024 yalikuwa 645 kulinganisha na kipindi  cha Julai 2024 hadi Juni, 2025 ambapo yameripotiwa 702.

Kuhusu hali ya uchumi,  Sirro alisema pato la mkoa limeongezeka kutoka Sh. trilioni 4.1 mwaka 2020 hadi Sh. trilioni 5.6 mwaka 2024 sawa na ukuaji wa asilimia 38.6.

Pia alisema  pato la mwananchi limeongezeka kutoka Sh.milioni 1.4 mwaka 2020 hadi kufikia Sh.milioni 2.1 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 45.4.

Aidha, alibainisha mafanikio mengine kuwa ni ujenzi wa bandari za Ujiji na Kibirizi ambao umefikia asilimia 98 na unafanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Balozi Sirro alisema ujenzi huo ulikabiliwa na changamoto ya bandari kujaa maji kutokana na mabadiliko ya tabianchi na mradi hiyo inatekelezwa na Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation (CR15G).

Alibainisha kuwa bandari ya Ujiji ujenzi unagharimu Sh. bilioni nane na Kibirizi  Sh. bilioni 16.5.

Pamoja na hayo alisema katika miradi ya kimkakati, wanaendelea na ukamilishaji wa ukarabati wa meli ya MT Sangara ambayo inatumika kubeba shehena ya mafuta lita 410,000 katika Ziwa Tanganyika ambao umefikia asilimia 99.

Alisema meli hiyo ni kiunganishi na tegemeo kwa shehena ya mafuta yanayosafirishwa Kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Burundi.

 “Tunaendelea na utekelezaji wa ukarabati wa meli kongwe ya MV Liemba yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 200 za mizigo ambao umefikia asilimia 15. Meli  hiyo inatarajiwa kutoa huduma ya usafiri kwa abiria na mizigo kwa wakazi waishio katika mwambao wa Ziwa Tanganyika,” alisema.

 Balozi Sirro alisema meli hiyo inatarajiwa kuongeza utalii kwa kuwa ni kivutio kikubwa kwa watalii wanaofika nchini kutokana na historia yake na kwa kuzingatia meli hii ni sehemu ya urithi wa taifa.

Sirro pia alisema wanaendelea na ujenzi wa Stendi ya Mabasi ya Kakonko kwa gharama ya Sh.milioni 351.4 na ujenzi wake umefikia asilimia 85.