Mawakili wa CHADEMA wapinga ufafanuzi wa amri ya Mahakama

By Jenifer Gilla , Nipashe Jumapili
Published at 01:45 PM Jul 20 2025
Mzani wa usawa kisheria
Picha: Mtandao
Mzani wa usawa kisheria

MAWAKILI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamesema barua ya ufafanuzi wa amri ya Mahakama Kuu iliyotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo ni batili, kinyume cha sheria na inalenga kupotosha uelewa wa umma kuhusu uamuzi halali ya mahakama.

Akizungumza kwa niaba ya mawakili hao, Wakili Hekima Mwasipu, alisema barua hiyo iliyoandikwa Julai 14, mwaka huu,  na kuelekezwa kwa mawakili wa chama hicho Julai 17,mwaka huu, imetafsiri vibaya amri mbili muhimu zilizotolewa na Mahakama Kuu, Juni 10, mwaka huu.

Katika amri hizo, Mahakama Kuu iliizuia Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu wa chama hicho kufanya shughuli za kisiasa na amri ya pili ilizuia bodi hiyo na Katibu Mkuu, wafanyakazi wao na mawakala wao  kutumia rasilimali za chama mpaka shauri la msingi litakaposikilizwa na kuamuliwa.

Mwasipu alidai barua ya Msajili imekiuka maudhui ya amri hiyo kwa kuorodhesha majina ya watu 10 waliodaiwa kuzuiwa, jambo ambalo haliko katika uamuzi wa mahakama.

Alitaja baadhi ya watu walioorodheshwa kwenye barua hiyo kuwa walizuiwa na amri ya mahakama ni pamoja na Mwenyekiti wa Taifa, Makamu Mwenyekiti Bara na Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu Bara na Zanzibar, na viongozi wengine wa chama, jambo ambalo si kweli.

Alidai barua hiyo pia haina jina la Naibu Msajili aliyetoa ufafanuzi huo, lakini imesajiliwa kwa neno ‘moyo’ ilhali mahakama hiyo ina Manaibu Wasajili takribani  wanne.

 Alisema majukumu ya msajili yako kwa mujibu wa sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai Sura ya 33 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.

Kwa mujibu wa wakili huyo, Amri ya 43 Kanuni ya Kwanza ya sheria hiyo imeorodhesha majukumu ya Msajili na hakuna popote inapoeleza kuwa Msajili anaweza kutoa tafsiri ya amri ya mahakama.

Mwasipu alisema pia kuwa hakuna ushahidi kwamba barua hiyo ya ufafanuzi ilitolewa kwa maelekezo ya Jaji Mkuu, ambaye kwa mujibu wa sheria ndiye mwenye mamlaka ya kumpa msajili majukumu maalum.

“Kisheria, hukumu ya mahakama inajieleza yenyewe. Msajili hana mamlaka ya kutoa tafsiri ya hukumu au amri ya mahakama. Hakuna kifungu cha sheria kinachompa uwezo huo”, alisema.

Wakili hao walisema wamekubaliana na wateja wao; Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika na Bodi ya Wadhamini kumwandikia  barua Naibu msajili kumweleza kuwa barua yake haina msingi wa kisheria na haina uhalali wowote.

Pia, wamemtaka aandike barua ya kuomba radhi kwa CHADEMA na kuikanusha barua yake ya awali au kukiri kuwa alikosea, vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

“Barua ya Naibu Msajili imepotosha kwa kiasi kikubwa. Amri ya mahakama ilikuwa wazi kwamba waliozuiwa ni Katibu Mkuu na Bodi ya Wadhamini pekee. Si viongozi wote kama ilivyodaiwa katika barua hiyo,” alisema Mwasipu.

Zuio hilo linalotokana na kesi namba 8323/2025 iliyofunguliwa na aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Issa na wenzake wawili ambayo imetolewa uamuzi na Jaji Hamidu Mwanga.