Arusha yapunguza vifo wajawazito kwa asilimia 78

By Paul Mabeja , Nipashe Jumapili
Published at 03:18 PM Jul 20 2025
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi
Picha: Paul Mabeja
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi

KATIKA kipindi cha miaka minne ya uongozi wa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, mkoa wa Arusha umefanikiwa kupunguza vifo vya wajawazito kwa asilimia 78, kutoka vifo 50 mwaka 2021 hadi vifo 11 mwaka 2025.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi, amesema hayo Julai 20 jijini Dodoma, wakati akieleza mafaniko ya mkoa huo katika kipindi cha uongozi wa serikali ya awamu ya sita kwa waandishi wa habari.

“Uboreshaji wa huduma za afya umerahisisha upatikanaji wa huduma za afya katika maeneo mbalimbali ndani ya mkoa wa Arusha na kuwezesha kupunguza vifo vya wajawazito kwa asilimia 78, kutoka vifo 50 (2021) hadi vifo 11 mwaka (2025).

Miongoni mwa wanahabari kwenye mkutano huo
“Lakini vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 859 mwaka 2021 hadi vifo 117 mwaka 2025 sawa na asilimia 86.4,”amesema Kihongosi

Amesema, pia kuanzishwa kwa Mfumo wa Rufaa wa M-Mama, kumesaidia jumla ya akina mama wajawazito 1,332 kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Aidha, amesema mkoa umetekeleza programu ya elimu bila malipo kwa gharama ya Sh. bilioni 168.2 wanafunzi walionufaika imeongezeka kutoka wanafunzi 390,910 (2021) hadi 430,511 (2025).