CAG: Mkandarasi alilipwa milioni 586/- za ziada

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 06:34 PM Apr 20 2025
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere
Picha: Mttandao
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, amesema amebaini Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) alimlipa mkandarasi malipo ya ziada kwa wakandarasi ya Sh.milioni 586.43.

Amesema katika ukaguzi wake alibaini Agosti mosi mwaka 2023, TANROADS ilimlipa Kampuni ya M/S China Civil Engineering Construction Company (CCECC) jumla ya Sh. 3,894,793,405.21 kwa madai ya malipo ya mkandarasi namba 1 (IPC Na. 1) chini ya Mradi wa Ushirikiano wa Usafiri Tanzania (TanTIP).

Katika malipo haya, nilibaini malipo ya ziada ya jumla ya Sh. 540,792,094 yaliyotokana na matumizi yasiyo sahihi ya fomula ya marekebisho ya bei.

Vilevile, katika Mradi wa Barabara ya Mkoa wa Iringa (Ipogolo - Kilolo), nilibaini jumla malipo ya ziada ya Sh. 45,640,034 katika Madai ya Malipo ya Wakandarasi Namba 2 na 3, ambayo yamehusisha Sh. 9,462,996 za uchimbaji wa miamba iliyokuwa imelipwa katika malipo ya ankara za nyuma.

Sh. 18,743,120 za vipimo vya maabara zilizotakiwa kulipwa na mkandarasi; na Sh. 17,433,918 zilizothibitishwa kimakosa kama kiasi cha malipo ya mkandarasi ya ada ya Bodi ya Kuepusha/Kusimamia Migogoro (DAAB).

“Ninapendekeza menejimenti ya TANROADS ipitie upya mchakato wa malipo na kuhakikisha kuwa hesabu za marekebisho ya bei zinazingatia kwa makini masharti ya mkataba, hususani matumizi sahihi ya fomula kama ilivyoainishwa katika kifungu kidogo cha 3.7.2 cha masharti ya jumla ya mkataba.

Aidha, wakala uwatakaje wakandarasi kurejesha fedha walizolipwa zaidi na kutekeleza mfumo wa kuthibitisha hesabu kabla ya kuidhinisha malipo katika miradi inayoendelea.