SIMBA SC: ITAWEZEKANA

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 02:30 PM Apr 27 2025
Kikosi cha Simba SC
Picha: Mtandao
Kikosi cha Simba SC

IMEFIKA, ile siku ambayo wanachama na mashabiki wa Simba wanahitaji kuona timu yao inakata tiketi ya kutinga fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika itakapowakabili wenyeji, Stellenbosch FC katika mechi itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Moses Mabhida, Afrika Kusini.

Mechi hiyo ya marudiano ya hatua ya nusu fainali itafanyika kuanzia saa 10:00 jioni kwa saa za Tanzania.

Simba itaingia uwanjani ikiwa na mtaji wa bao 1-0 iliopata Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, katika mchezo wa mkondo wa kwanza.

Kwa hesabu rahisi, Mnyama atakuwa na kazi moja tu ya kulinda ushindi wake kwa kulazimisha sare yoyote au kupata ushindi mwingine ikiwa huko ugenini.

Simba imepania kufanya kile ilichokifanya mwaka, 1993 huko Angola, ilipolazimisha suluhu dhidi ya Atletico Sport Aviacao katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la CAF, ambalo sasa linaitwa Kombe la Shirikisho, baada ya ushindi wa mabao 3-1 iliyovuna kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam (sasa Uhuru), kwa mabao mawili ya Edward Chumila na Malota Soma, wageni wakipata bao lao kupitia kwa Nelo Miguel.

Katika mchezo wa leo, Simba itaendelea kukosa huduma ya beki wake wa kati, Fondoh Che Malone, ambaye ameanza mazoezi ya timu hiyo akitoka kwenye majeruhi, na taarifa zinasema bado anatakiwa awe na utimamu wa mwili sawa ili aanze kuingia kikosini taratibu na si kwenye mchezo mkubwa wenye presha kama huo.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema wamekwenda Sauzi kwa lengo moja tu kuhakikisha timu hiyo inatinga fainali.

Fadlu alisema kila kitu kilichotokea kwenye mchezo uliopita wamekiacha nyuma, badala yake wamepanga mpango mkakati wa kuhakikisha wanaimaliza mechi ya leo.

"Tumekuja na mpango mkakati wetu, tutashambulia kwa pamoja na kulinda kwa pamoja. Katika mchezo huu lengo ni kupata bao moja ambalo nadhani ndiyo litaua mechi yote.

Ili watutoe ni lazima watufunge matatu kama tukipata bao moja, hicho kitakuwa ni kipaumbele chetu cha kwanza katika mechi hii na tunalihitaji haraka sana ndani ya dakika 20 hivi, tukilipata basi tutacheza bila presha, kama hatulipati tutaendelea kuwasukuma wapinzani wetu ambao najua hata wao watacheza kwa uangalifu zaidi," alisema Fadlu.

Alisema kitu ambacho anajivunia ni kumaliza dakika 90 za nyumbani Zanzibar bila kuruhusu bao.

"Kumbuka, kama tungeshinda mabao mawili, halafu tukaruhusu bao moja, tungekuwa kwenye hali ya hatari zaidi kwa sababu hata wakishinda goli 1-0 wangekuwa wametumaliza, kwa sasa hali siyo ilivyo," alisema kocha huyo.

Aliongeza wapinzani wao ni moja ya timu hatari, hivyo wataingia uwanjani kwa tahadhari pia.

"Stellenbosch ni timu ya kuogopewa, wameshawafunga Sundowns (Mamelodi), Pirates (Orlando) na waliipa changamoto Kaizer Chiefs, wanajua namna ya kucheza dhidi ya timu kubwa. Hawajali watamiliki mpira kwa kiwango gani, lakini wao wakipata nafasi moja wanaitumia vyema kulazimika matokeo chanya," Fadlu alisema.

Kocha huyo alisema wachezaji wake wako tayari na kamili kumalizia kazi waliyoianza nyumbani na si vinginevyo.

Mechi hiyo imeonekana kuvuta hisia za mashabiki wa soka wa Afrika Kusini, hususan watanzania wanaoishi huko ambao wamekuwa wakiandamana na kikosi kila kinakokwenda, wakiahidi kuiunga mkono na kuishangilia kwa nguvu katika mchezo huo.

Balozi wa Tanzania nchini humo, James Bwana, amesema baadhi ya watanzania wanaoishi nchi za jirani kutoka Namibia, Msumbiji, Zimbabwe, Botswana, Eswatini, Angola na Zimbabwe, wamewasili Afrika Kusini kwa ajili ya kuishangilia Simba.

Bwana alisema huenda Simba leo ikawa na idadi kuwa ya mashabiki kuliko wenyeji wao kutokana na mwamko mkubwa uliojitokeza.

Simba ilitinga hatua hiyo kibabe ikitoka nyuma kwa mabao mawili, hadi kupata ushindi kama huo nyumbani na kuwafunga Al Masry ya Misri penalti 4-2 huku Stellenbosch ikiwaondoa mabingwa watetezi, Zamalek kwa ushindi wa bao 1-0 wa ugenini baada ya matokeo ya suluhu kwenye mchezo wa kwanza.