Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umetoa elimu kuhusu huduma unazotoa katika Semina ya Kuwajenega Uwezo Wafanyakazi Vijana ambao ni wanachama wa chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri.
Semina hiyo imefanyika Aprili mjini Singida ambapo, Afisa Mafao Mkuu wa PSSSF, Ramadhani Sossora, amewaambia washiriki kuwa, PSSSF ina majukumu makuu manne ambayo ni pamoja na Kusajili Wanachama, Kukusanya Michango, Kuwekeza na Kulipa Mafao.
Aidha, amewaambia kuwa PSSSF inalipa jumla ya Mafao saba ambayo ni pamoja na Fao la Uzeeni, Fao la Wategemezi, Fao la Kifo, Fao la Kukosa Ajira, Fao la Ulemavu, Fao la Ugonjwa na Fao la Uzazi.
Kuhusu Uwekezaji, Sossoro amesema, PSSSF imewekeza kwa kufuata muongozo wa Benki Kuu ya Tanzania na kutaja maeneo iliyowekeza ni pamoja na kwenye Hatifungani za Serikali, Majengo ya Biashara na Makazi lakini pia kwenye viwanda.
Kuhusu utoaji wa huduma, alisema, Mfuko umefanya mapinduzi makubwa ya utoaji w ahuduma zake ambapo kwa sasa huduma zote zinatolewa kupitia mtandao maarufu PSSSF Kidijitali.
Kupitia PSSSF Kidijitali, Mwanajiri anaweza kuwasilisha michango.
Lakini pia PSSSF Kidijitali inamuwezesha mwanachama kupitia simu janja, kishikwambi au computer kujihudumia yeye mwenyewe kama vile kupata Taarifa za Michango, Taarifa za Uwekezaji, Kuwasilisha Madai na kwa Wastaafu wanaweza kujihakiki kupitia simu janja.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED