‘Sekta sukari inaendelea kuwa himilivu’

By Ida Mushi , Nipashe Jumapili
Published at 03:52 PM Apr 27 2025
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari, Prof. Kenneth Bengesi, akizungumza na waandishi wa habari
Picha: Idda Mushi, Morogoro
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari, Prof. Kenneth Bengesi, akizungumza na waandishi wa habari

MKURUGENZI Mkuu wa Bodi ya Sukari, Prof Kenneth Bengesi, amesema Tanzania iko mbioni kuondokana na uhaba wa sukari, kutokana na uwekezaji unaoendelea.

Amesema hayo wakati wa kongamano la wadau wa sukari lililoandaliwa na Jumuiya ya chama cha wataalamu wa Miwa na Sukari nchini (TSSCT) katika chuo cha Sukari cha Taifa, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro.

Aidha, wadau mbalimbali wakiwamo wataalamu wa sasa na wa zamani wa miwa na sukari, menejimenti za viwanda vya sukari, bodi, mfuko wa maendeleo ya sukari, wazalishaji wa teknolojia, vyama vya wakulima na wengine, wameshiriki.

Mkurugenzi mkuu huyo, amesema eneo la sukari imeendelea kuwa na maendeleo makubwa hasa katika kipindi cha awamu ya sita, kutokana na changamoto mbalimbali zilizokuwapo kutatuliwa.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Uendelezaji wa Teknolojia na Ushirikiano wa Kitaaluma kutoka TARI, Dk. Sophia Kashenge
“Licha ya mwaka jana mvua za Elnino kuondoa utulivu kwa kuvuruga mifumo ya uzalishaji na miundo ya mashamba, sasa utulivu umeendelea kuwapo kwa upatikanaji wa sukari umekuwa wa uhakika nchi nzima, kuna utulivu wa bei hali inayotoa tumaini kuwa walaji kuwa na uhakika wanapata kwa bei himilivu na wawekezaji wanafanya biashara yao kwa utulivu,” amesema Prof. Bengesi.

Akasema lengo la serikali sio kujitosheleza kwa sukari peke yake, bali pia kuzalisha ziada itakayouzwa nje ya nchi na kupata uhakika wa fedha za kigeni zitakazotumika kutatua changamoto za kijamii na kujenga miundombinu ya kiuchumi.

“Utulivu uliopo kwa miaka ya karibuni umewezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa sukari kutoka tani 295,000 miaka saba, nane iliyopita kufikia tani 460,000 zilizorekodiwa mwaka juzi ikiwa ni kiasi cha juu kabisa kwa karibu mara mbili zaidi ya uzalishaji uliokuwapo.

Rais wa Jumuiya ya Chama cha Wataalamu wa Miwa na Sukari Tanzania TSSCT, Fihiri Achi
“Upanuzi wa mashamba, ili yazalishe malighafi ya kutosha na kwenda sambamba na upanuzi wa viwanda na hata wakulima wadogo kutengenezewa mazingira mazuri ya kulima kwa tija,” ameongeza.

Amesema kwa sasa pia serikali inatoa ruzuru ya mbolea na kuongeza uzalishaji wa miwa sambamba na kurahisisha upatikanaji wa mitaji, kwa kuongea na mabenki na kuweka mazingira mazuri ya mikopo.

Katibu wa Jumuiya ya Chama cha Wataalamu wa Miwa na Sukari Tanzania (TSSCT), Mwanaidi Jaffery, amepongeza jitihada za seriikali kwenye sekta ya sukari na kusaidia uhimilivu, kuongeza uzalishaji wa miwa na sukari na kuziba uhaba wa sukari.

Wataalamu wa sukari na miwa waliokutana kwenye kongamano maalum la sekta ya sukari katika chuo cha taifa cha Sukari, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro
“Tumeendelea kuwa chachu ya kuchagiza tafiti katika tasnia ya sukari na miwa kwani imani yetu ni kuwa bila tafiti nchi haiwezi kuwa na bunifu zitakazoibua uzalishaji wa mbegu bora na uzalishaji wa teknolojia kusaidia kuongeza uzalishaji,” amesema.

Rais huyo wa TSSCT akasema wao kama wataalamu wamekuwa wakihusika mashambani na viwandani hivyo  wamegundua bado kuna changamoto ya matumizi madogo ya TEHAMA, kwa upande wa wakulima wadogo, kumechangia wakulima kupata tija ndogo.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Uendelezaji wa Teknolojia na Ushirikiano wa Kitaaluma kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Dk. Sophia Kashenge, amesema licha ya changamoto nyingi katika sekta ya sukari, bado sekta hiyo imeendelea kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.