MTUME Boniface Mwamposa wa Kanisa la Inuka Uangaze, amesema watanzania waliombee taifa, ili liwe na amani kuelekea uchaguzi mkuu, mwaka huu.
Mwamposa amesema hayo katika ibada ya Pasaką, kwenye kanisa hilo, Dar es Salaam, akisema sikukuu hiyo ya ufufuko wa Yesu ni wokovu, uponyaji, ushindi, maangamizo na amani, hivyo katika taifa la Tanzania kitu pekee cha kulilinda ni amani.
Tutaendelea kuliombea taifa na kila mmoja ainue taifa. Yesu anaitwa mfalme wa amani na ukiona tumekaa hivi na kusherehekea kufufuka kwa Yesu basi Mungu ametupa amani," amesema.
Mwamposa ameeleza kwamba Yesu aliwaambia wana wa amani kuwa wakiingia nyumba yoyote waseme amani iwe ndani ya nyumba hiyo, hivyo lazima amani itaishi, pasipokuwapo itaondoka kwa maana inatembea na inahitaji kiti ikae.
“Kipindi cha uchaguzi kina mambo mengi, adui anafungulia mlango. Tunamshukuru Mungu kwa Taifa letu naendelea kuliombea amani na tukaendelee kuilinda amani iliyopo," amesema.
Amesema amani ni muhimu kwa kuwa watu hawawezi kukaa kwa pamoja kusali pasipo amanai, hivyo maombi ni muhimu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED