Watu 755, wakiwamo watoto 21 wachunguzwa moyo Sabasaba

By Christina Mwakangale , Nipashe Jumapili
Published at 12:59 AM Jul 06 2025
Mtaalam akimhudumia mtoto aliyefika Banda la JKCI Sabasaba
Picha: JKCI
Mtaalam akimhudumia mtoto aliyefika Banda la JKCI Sabasaba

WATU 755 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), lililopo kwenye Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF).

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa magonjwa yatokanayo na kazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Dar Group, Elius Birago amesema kati ya watu waliowaona kwa muda wa siku saba wanaume walikuwa wengi zaidi ukilinganisha na wanawake.

Dk. Birago amesema wanaume waliowaona walikuwa 415, wanawake 319 na watoto 21 huku wengi wao wakiwa na matatizo ya shinikizo la juu la damu, kisukari na kuna ambao hawakujijua kabisa kuwa na tatizo hilo lakini baada ya kupata vipimo wamekutwa na shida.

“Katika maonesho ya mwaka huu wanaume wamejitokeza kwa wingi zaidi kupima afya zao ukilinganisha na mwaka jana ambapo wanawake walikuwa wengi zaidi, maonesho haya yamekuwa na faida kwao kwani wamepewa ushauri na wengine wamepata rufani, kwa ajili ya kuanza kliniki”, amesema Dk. Birago.

“Kuna ambao walikuwa wanapita njia baada ya kuona tuko hapa wakaja kupima afya za mioyo yao, kuna ambao tumewakuta na dalili za saratani tumewaelekeza waende banda la Taasisi ya Saratani Ocean Road na wengine tuliowakuta na  dalili za magonjwa mengine tumewaelekeza waende katika banda la Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Dk. Birago almewaomba wananchi watumie maonesho hayo kupima afya zao pia wawe na tabia ya kupima afya ya moyo mara kwa mara kwani ugonjwa wa shinikizo la juu la damu hauna dalili na wengine wanapata wakati tayari wameshapata madhara ya ugonjwa huo.

Kwa upande wa wananchi waliopata huduma katika banda hilo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kujua hali zao na kuokoa muda wa kuifuata huduma hiyo hospitali.

“Nilisikia katika vyombo vya habari kuwa huduma za upimaji wa moyo zinatolewa katika banda hili nami nikaona nije kupima ingawa nilikuwa na hofu ya kutumia muda mwingi kusubiri kupata huduma, lakini nimetumia muda mfupi kupima na nimeandikiwa dawa za kutumia”, amesema Jackson Urio mkazi wa Kigamboni.