RAIS Samia Suluhu Hassan amehimiza wananchi kuendelea kuzalisha zaidi mazao ya chakula na biashara na kuahidi serikali kuendelea kuwatafutia masoko ya uhakika.
Rais Samia alisema hayo jana akiwa wilayani Gairo, mkoani Morogoro ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku sita mkoani humu, akimwagiza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuweka mikakati itakayowezesha mbaazi kupata soko na bei nzuri kama ilivyo kwa korosho kwa mikoa ya kusini.
Akizungumza na wananchi baada ya kuzindua Hospitali ya Wilaya ya Kilosa na baadaye Daraja la Berega linalounganisha wananchi na Hospitali ya Berega, Rais Samia alisema anajua zao la mbaazi halina bei nzuri sokoni ndio maana anataka jitihada za makusudi kupata soko na bei ya uhakika.
Alisema amefika Morogoro pamoja na mambo mengine kusikiliza shida za wananchi na kuzifanyia kazi, kuona matokeo ya fedha za maendeleo zinazotolewa, kuzindua, kukagua na kuweka jiwe la msingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuangalia urejeshwaji miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko kutokana na mvua ya El- Nino.
Rais Samia aliyeridhishwa na matumizi ya fedha katika ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Gairo, aliwataka wananchi mkoani Morogoro kujipanga kwa ajili ya Uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa na kuzingatia kuchagua viongozi bora ili kufikiwa na maendeleo.
Kuhusu changamoto ya maji wilayani Gairo, Mkuu wa Nchi alisema iko mbioni kutatauliwa baada ya serikali kutoa Sh. bilioni 34 kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji; mikataba imeshatiwa saini.
Alisema kuwa Wilaya ya Gairo inakwenda kuondokana na changamoto ya kukatika ovyo kwa umeme baada ya serikali kujenga kituo cha kupokea, kupooza na kusambaza umeme katika wilaya jirani ya Kongwa, mkoani Dodoma.
"Gairo mna bahati sana kama alivyosema Mbunge wenu (Ahmed Shabiby), changamoto zote zilizokuwa zimeahidiwa zimetatuliwa na hizi zilizotajwa hapa pia zote tutakwenda kuzifanyia kazi.
"Niko na mawaziri wangu na wakati mbunge wenu anazitaja niliona kila mmoja ana kalamu, anaziandika vizuri," alisema Rais Samia aliyeongozana na mawaziri 10 na wasaidizi wao wizarani.
Awali Mbunge wa Gairo, Shabiby, alipongeza serikali chini ya Rais Samia kwa kutekeleza ahadi nyingi hasa zilizoahidiwa na Rais ndani ya kipindi cha miaka mitatu na nusu aliyokaa madarakani ikiwamo ujenzi wa Kituo cha Afya Nongwe, Magereza na Mahakama.
Mafanikio mengine aliyataja ni utekelezaji wa ahadi ya ujenzi wa madaraja mawili moja lenye urefu wa mita 80 na lingine urefu wa mita 100 ambayo yana uwezo wa kupita magari mawili yanayounganisha na barabara ya lami ya kwenda Kilindi sambamba na mfereji mkubwa wa kuzuia mafuriko.
Alisema kuwa hivi sasa barabara zote za Gairo zinapitika hadi milimani na kuna mawasiliano ya simu na miundombinu ya barabara.
Alisema serikali ilitoa zaidi ya Sh. bilioni 18 kwa ajili ya miradi ya elimu na afya na kuomba serikali kuongeza fedha zaidi kwa ajili ya dawa na gari la wagonjwa wa dharura kutokana na eneo hilo kuhudumia wananchi wa Kiteto na Kilindi na limekuwa likipokea majeruhi wa ajali mara kwa mara katika barabara kuu ya Morogoro-Dodoma.
"Tunaomba serikali itupatie pia ruzuku ya mbegu za alizeti kwa wananchi na itujengee soko la kisasa na stendi (kituo cha mabasi) ya wilaya," alisema.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa, alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu na nusu ya Rais Samia, mambo makubwa ya kizalendo yamefanyika na kugusa maisha ya Watanzania wa hali ya chini ikiwamo katika sekta za elimu na afya.
Alisema kwa Wilaya ya Gairo, zahanatii mpya 32 zilijengwa pamoja na hospitali ya wilaya iliyogharimu zaidi ya Sh. bilioni tisa ambayo haikuwapo awali.
"Kwa kipindi hiki tu cha miaka mitatu karibu na nusu chini ya uongozi wako Mheshimiwa Rais, zaidi ya wananchi 12,335 wamepata huduma katika hospitali hii, lakini kuna wagonjwa wa dharura zaidi ya 700.
"Fedha zinazotolewa na serikali zimesogeza huduma karibu kabisa na wananchi wakiwamo wananchi wanyonge, kazi hizi zote zinatosha kukunadi," alisema Waziri Mchengerwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED