TGNP yatoa angalizo udhalilisha wanawake kwenye kampeni

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 07:04 PM Nov 20 2024
kuu wa Program Mafunzo  kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Anna Sangai
Picha: Grace Mwakalinga
kuu wa Program Mafunzo kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Anna Sangai

MTANDAO WA Jinsia Tanzania (TGNP), umewataka wagombea wa vyama mbalimbali kufanya kampeni zinazozingatia, haki na utu wa mwanamke na kuepuka udhalilishaji unaofanywa na baadhi ya wagombea majukwaani kwa kundi hilo.

Wito huo, ulitolewa leo na Ofisa Program wa  Mafunzo  wa Mtandao huo, Anna Sangai, wakati akizungumza na Nipashe kuhusu mambo yanayopaswa kuzingatiwa kipindi hiki cha uchaguzi.

Amesema ni muhimu kampeni zikafanyika kwa amani na utulivu ili kulinda haki za binadamu hususani wanawake ambao wamekuwa wakiathiriwa na lugha za uzalilishaji kwenye kipindi cha uchaguzi.

“ Tunaviomba vyama vya siasa kuzingatia utu wa mwanamke katika mikutano yao, sisi kama watetezi wa haki  na usawa wa kijinsia, hatupendi udhalilishaji  dhidi ya mwanamke majukwaani au katika eneo lolote wakati wa kampeni, tumejipanga kushiriki kikamilifu  ili  tushinde nafasi mbalimbali,” amesema Anna.

Ameongeza kuwa ni muhimu vyama vya siasa vikatoa muda sawa kati ya wanaume na wanamke wakati wa kunadi sera, sambamba na vyombo  vya ulinzi na usalama, kuwapo maeneo yote yanayofanyika mikutano ya kisiasa kuimarisha ulinzi bila kujali aina ya vyama hivyo.

“Uwapo wa vyombo vya ulinzi na usalama kwenye maeneo yote yanayofanyika kampeni itasaidia wanawake kujiamini na kumwaga sera zao kwa wapiga kura, kwa sababu asilimia kubwa ya wanawake hao hawana uwezo wa kumuajiri walinzi binafsi,” amesema Anna.

Tayari Kampeni za uchaguzi huo wa serikali za mitaa zimeanza leo na kushuhudia viongozi wakuu wa vyama tofauti wakizindua rasmi kampeni hizo, kwenye mikoa mbalimbali nchini.