KWA miaka mingi nchini, migogoro kuhusu mirathi na kugombea mali katika familia mbalimbali imekuwa ikiongezeka hata kusababisha baadhi ya wahusika kuuawa au kupata ulemavu wa kudumu.
Chanzo kikubwa cha kuwapo kwa madhila hayo ni Watanzania wengi kushindwa kuandika wosia wakati wakiwa hai. Hatua hiyo husababisha kuibuka kwa migogoro ndani ya familia kutokana na kugombania mali za marehemu na wakati mwingine mama na watoto, mara baba anapoaga dunia, hufukuzwa kwenye nyumba na kuporwa mali na baba wadogo, wakubwa na mashangazi.
Kwa familia zile ambazo zimekuwa zikisimama imara na kuweka misimamo dhidi ya ndugu wa marehemu kuchukua mali hizo, zimekuwa zikifanyiwa mauaji yakiwamo ya kinyama kwa kuchomwa moto na kuteketea wakiwa ndani ya nyumba. Matukio hayo yamejitokeza kwa kiasi kikubwa katika baadhi ya makabila yanayoendekeza mfumo dume kwamba mwanamke hawezi kurithi mali za mume.
Sababu kubwa au kasumba iliyoenea miongoni mwa Watanzania kutokuandika wosia ni imani katika jamii kwamba kufanya hivyo ni uchuro. Wako baadhi ya watu ambao wanaamini kwamba kuandika wosia ni kujitabiria kifo.
Licha ya kuwapo kwa madhara hayo, baadhi ya familia zimekuwa zikipata matatizo kama vile watoto kukatisha masomo kutokana na akaunti za wazazi kusimamishwa hadi mrithi atakapopatikana. Hali hiyo husababishwa na migogoro na mashauri ya mirathi kuchukua muda mrefu kwa sababu ya kuwapo kwa mivutano katika baadhi ya familia baina ya ndugu upande mmoja na mke na watoto wa marehemu upande mwingine.
Mbali na mivutano hiyo, wako baadhi ya watu ambao wamekuwa wakichukua mali za marehemu kwa nguvu na wakati mwingine, kutokana na mashauri ya mirathi kuchukua muda mrefu, baadhi ya mali zimekuwa zikipotea au kuharibika. Jambo hilo husababisha hasara kwa baadhi ya wanafamilia kwa kuwa mali hizo zingewawezesha kuzitumia kwa makusudi mbalimbali.
Kuwapo kwa hali hiyo, kumesababisha serikali na wadau mbalimbali, wakiwamo wanaharakati wa kutetea haki za binadamu kutoa elimu kuhusu umuhimu wa watu kuandika wosia. Jitihada hizo zimekuwa sawa na kutwanga maji kwenye kinu kwa kuwa mwitikio umekuwa mdogo.
Jambo la kufurahisha ni kwamba serikali haijakata tamaa katika kuwahimiza watu kufanya hivyo. Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini, ameendeleza jitihada za serikali kutaka elimu hiyo itolewe kwa wananchi ili kujua muhimu wa kuandika wosia. Katika kufanya hivyo, ameshauri itafutwe njia ya kuwasaidia wananchi kuondoa hofu ya kutokuandika wosia ili kupunguza migogoro kipindi cha mirathi.
Akiwa katika ziara kwenye Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali na kuona shughuli za kimahakama zinazotolewa kwa wananchi jana, Sagini alisema hali hiyo inatokea kwa sababu wananchi wengi hawaelewi umuhimu wa wosia. Kutokana na hali hiyo, alisema elimu bado inatakiwa kutolewa katika jamii ili kuondoa mgongano au kutofautiana kwa wanafamilia.
Kurudiwa kwa msisitizo huo kuhusu elimu na mwitikio kuwa mdogo imekuwa sawa na maagizo muhimu kutolewa na hatimaye kufikia katika masikio ya viziwi. Kwa maneno mengine, imekuwa sawa na viongozi wa dini kuwataka waumini wao kuacha dhambi na wao kusikia na kuendelea na mambo hayo kama kawaida.
Ni dhahiri kwamba tatizo la watu kushindwa kuandika wosia limekuwa sugu kwa sasa ndiyo maana kuna migogoro mingi ndani ya familia za kitanzania. Kama ni ngoma kuhusu mirathi imepigwa kwa kiasi kikubwa, hivyo ni muhimu kwa Watanzania kutekeleza ushauri huo kwa maisha yao.
Kama wahenga wasemavyo asiyesikia la mkuu huvunjika guu, vivyo hivyo kuendelea kupuuza ushauri kuhusu kuandika wosia ni sawa na kukubali kuingia katika matatizo licha ya kuambiwa mara kwa mara. Shime Watanzania wasikie wito huo na kuufanyia kazi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED