TAASISI ya Uongozi juzi ilifanya mahafali ya saba yaliyojumuisha wahitimu 198 wa kozi ya uongozi kutoka taasisi mbalimbali za serikali na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete alikuwa mgeni rasmi.
Katika hotuba yake, Kikwete alitoa wosia mzito si kwa wahitimu hao tu bali kwa viongozi walioko kwenye taasisi za serikali na binafsi ambao majukumu yao ya kila siku ni kuhudumia wananchi na kuwaletea maendeleo. Kikwete aliwashauri wahitimu hao kuwa na mipango na mawazo yatakayosaidia kuacha alama katika uongozi wao pale watakapoacha au kuhamishwa.
Kiongozi huyo ambaye amejijengea sifa kubwa katika uongozi tangu enzi za ujana wake, alisema ni muhimu kwa viongozi wawe na mipango kabambe kwa taasisi wanazoongoza na kwa nafasi zao ili watakapomaliza wakumbukwe kwa mazuri waliyofanya kwa kizazi cha sasa na vijavyo. Alisisitiza kwamba jambo ambalo wanapaswa kulipa kipaumbele kwenye nafasi zao za uongozi ni namna watakavyokumbukwa baada ya maisha ya uongozi na ni alama gani wataiweka ambayo haitafutika miaka mingi.
Licha ya kufanya hivyo, alisisitiza kuwa wanapaswa kuwa chimbuko la mawazo katika kutekeleza majukumu yao na pia kuwa chanzo cha mabadiliko katika ngazi mbalimbali wanazozitumikia. Pia alisema viongozi wanapaswa kuwa tayari kutafuta suluhu za changamoto zinazoendelea kama vile umaskini, mabadiliko ya tabianchi, ujinga, njaa na maradhi.
Wahenga wanasema uzee ni dawa. Maneno ya kiongozi huyo aliyeshika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama tawala na serikali pamoja na kuwa nyota katika medani ya kimataifa, yanasadifu na ukweli kuhusu uongozi. Kiongozi siku zote anapaswa kuwa mbunifu na mstari wa mbele katika utekelezaji wa mawazo yake pamoja na kutatua changamoto zinazoihusu taasisi na jamii inayomzunguka.
Jambo hilo katika uhalisia wa sasa limekuwa kama msamiati mgumu kwa baadhi ya viongozi wa sasa. Idadi kubwa ya watu wanaoingia katika uongozi hawafikirii changamoto au matatizo yanayowasibu wananchi au jamii bali matamanio na mipango binafsi. Matokeo yake, wanashindwa kuleta mabadiliko chanya kupitia nafasi wanazopewa katika uongozi.
Kutokana na ukweli huo, watu wengi wanaosaka nafasi za uongozi wanatumia fedha ili kuzipata na kuna msemo uliozoeleka katika jamii ya sasa kwamba bila pesa ni vigumu kupata uongozi na mkono mtupu haulambwi. Kwa mantiki hiyo, wanatumia fedha kuanzia uongozi wa serikali za mitaa hadi serikali kuu kwa matumaini kwamba watavuna faida kutokana na ‘uwekezaji’ kwenye kura.
Katika miaka ya 1990 na 2000 waliokuwa wabunge wawili katika mkoa wa Dar es Salaam, waliwahi kuliliwa shida na wapigakura wao kuhusu kero za maji na majibu waliyotoa ni kwamba ubunge waliupata kwa fedha zao na si hisani ya wananchi hao. Huo ndio ukweli na ndiyo maana watu kama hao wanapoingia kwenye nafasi yoyote ya uongozi, mawazo yao ni kujineemesha wao na wale wanaowazunguka.
Ni wakati mwafaka sasa kwa viongozi, katika nafasi yoyote, kubadilisha fikra zao na kurejea maneno ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere, kwamba uongozi ni dhamana ya kuwatumikia watu na si kutumikiwa. Kama alivyosema Kikwete viongozi wafanye mambo yatakayosaidia kutatua kero zinazowakabili wananchi ili waache alama pindi watakapoondoka.
Waasisi wa taifa la Tanzania, Mwalimu Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, walitambua kuwa wamepewa dhamana ya kuwaongoza Watanzania kwa kuwatatulia kero zinazowakabili. Kwa kutambua na kutekeleza hayo, viongozi hao japokuwa wametangulia mbele ya haki, wameacha alama isiyofutika kwa vizazi vingi ndiyo maana mpaka sasa wanaendelea kukumbukwa.
Kwa mantiki hiyo, viongozi wa sasa na wajao, wanapaswa kuzingatia kauli ya Mzee Kikwete kuhusu dhana ya uongozi ili wakumbukwe baadaye kwa kazi zao njema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED