KWA muda mrefu kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara kuhusu masuala mbalimbali kutoka kwa watumishui wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) miongoni mwa malalamiko hayo ni madai ya kubambikiwa kodi, watumishi wa mamlaka hiyo kuwaomba rushwa wafanyabiashara huku wakiwatishia kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kuwa wanakwepa kodi na matumizi ya nguvu katika kudai kodi.
Katika miaka ya karibuni kwa mfano, baadhi ya wafanyabiashara walilalamika mbele ya viongozi wakuu wa serikali kwamba baadhi ya wafanyakazi wasio waaminifu wa TRA wamekuwa wakichukua mizigo yao kwa nguvu na kuificha kusikojulikana, hali ambayo huwasababishia hasara.
Hali hiyo ilizidi kuwa mbaya hivi karibuni baada ya wafanyabiashara kufunga maduka yao kwa madai kama hayo kuwa wananyanyaswa na maofisa wa TRA ambao wamekuwa wakiwabambikia kodi au kufanya makadirio ya juu tofauti na thamani ya bidhaa. Hatua hiyo ilisababisha si tu wafanyabiashara kupata hasara bali serikali kukosa mapato ikizingatiwa kwamba sehemu kubwa ya mapato ya serikali ambayo ndiyo bajeti halisi, hutokana na makusanyo ya kodi.
Baada ya migomo hiyo iliyotikisa katika mikoa mbalimbali, serikali ilikubali kukutana na wafanyabiashara hao, wakiwakilishwa na wenzao wa Kariakoo ambao walitoa madukuduku yao mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye aliahidi kuyafanyia kazi. Mkutano huo wa wafanyabiashara na serikali pia ulisababisha mabadiliko ndani ya TRA ambayo yalimgusa mtendaji mkuu wa mamlaka hiyo.
Nuru ya kuweka mazingira bora kwa wafanyabiashara na kuondoa kero zao imeanza kuonekana baada ya juzi, TRA kutangaza kuanza kutatua migogoro ya wafanyabiashara kwa kuweka utaratibu wa kukutana nao mara tatu kwa mwezi ili kuwasikiliza.
Kamishna Mkuu wa TRA, Yussuph Mwenda, wakati akizindua APP (application) ya TRA Sikika’, kwa ajili ya kupokea maoni, ushauri na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi ambayo yatamfikia Kamishana Mkuu moja kwa moja, alisema pamoja na kupokea maoni hayo, atakuwa anakwenda kukutana na wafanyabiashara hao na kufanya mazungumzo ambayo kwa kiasi kikubwa yataondoa kero nyingi zilizopo sasa.
Mwenda alisema wafanyabiashara wa Kariakoo, mathalan, miongoni mwa mambo yaliyojitokeza katika kikao na Waziri Mkuu hivi karibuni ni kuingiza mizigo kutoka nje kwa kuchangia na mtu mmoja kulipia ushuru wa forodha. Katika kutatua hilo, alisema mamlaka imeshatengeneza timu kwa ajili ya kutatua kero hiyo.
Kabla ya kufikia hatua ya kuanza kukutana, Mwenda pia alisema masuala ya makadirio ya ushuru wa forodha yameshaanza kupatiwa ufumbuzi na hivi sasa mfanyabiashara wa vitenge anajua kiwango cha ushuru anapoagiza bidhaa hiyo.
Jambo la kufurahisha ni kwamba Mwenda mpango wa serikali, kama alivyosema Mwenda, ni kuifanya Kariakoo kuwa soko la kimataifa na lenye ushindani katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara huku akiweka bayana kwamba haipendezi kuita soko la kimataifa wakati watu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) hawafiki na kununua bidhaa.
Ni wazi kwamba TRA imedhamiria kwa dhati kuhakikisha kunakuwapo mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara kufanya shughuli zao, hivyo kuiwezesha serikali kupata mapato stahiki.
Hatua ya kuweka utaratibu wa kukutana na wafanyuabishara ni mwafaka na umo katika 4R za uongozi wa Samia ambao unataka kuwe na maridhiano baina ya pande husika.
Kwa hiyo kukaa na wafanyabiashara na kuzungumza ni hatua itakayowezesha pande husika (TRA na wafanyabiashara) kuzungumza na hatimaye kufikia mwafaka utakaowezesha kuongezeka kwa mapato ya serikali.
Wahenga wanasema utamkamuaje ng’ombe maziwa ilhali humpi mashudu? Ndivyo ilivyo kwa wafanyabiashara wanavyotakiwa kuwekewa mazingira bora ya ufanyaji shughuli zao ili kulipa kodi halali na stahiki kwa maendeleo ya taifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED