RAIS wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Magufuli, baada ya kuingia madarakani, alisisitiza ulipaji wa kodi kwa wafanyabiashara na kuapa kuwa asingekuwa na msamaha na watu wanaokwepa kodi. Alikwenda mbali zaidi kwa kusema wakwepaji wa kodi ni maadui wakubwa wa maendeleo.
Kiongozi huyo aliziishi kauli zake hizo na kuwataka wafanyabishara, kundi ambalo ndilo hutuhumiwa kuwa wakwepaji wakubwa wa kodi, wanapofanya shughuli zao wahakikishe wanatoa risiti. Pia aliwasisitiza wananchi wanaponunua bidhaa kwa wafanyabiashara wadai risiti inayoonyesha kiasi halali cha fedha walichotumia kununulia bidhaa husika.
Aidha, ili kuhakikisha wauzaji na wanunuzi wa bidhaa husika wanatekeleza hilo, alianzisha usemi kwamba “Ukiuza Toa Risiti, Ukinunua Dai Risiti” na katika kutekeleza hilo, alisisitiza matumizi ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD).
Hatua hiyo ilisababisha makusanyo yatokanayo na kodi kuongezeka na hatimaye serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Sambamba na matumizi ya mashine hizo kwa wafanyabiashara, serikali ilianzisha mfumo wa ukusanyaji mapato serikalini na mamlaka za serikali za mitaa, kutumia mashine za aina hiyo (POS) na malipo kwa njia ya mtandao ili kudhibiti ufujaji wa fedha za umma.
Katika uhalisia wa maisha, wahalifu au wakiukaji wa sheria ambao kwa kufanya hivyo hunufaika, hubuni mbinu mpya za kuendeleza maovu au kutenda mambo ambayo ni kinyume cha sheria.
Pamoja na nia hiyo nzuri ya serikali kuhakikisha wafanyabiashara wanalipa kodi kama inavyotakiwa, baadhi ya wafanyabiashara wameibuka na mbinu mpya ambayo inasababisha serikali kushindwa kukusanya mapato kwa mujibu wa malengo inayojiwekea kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania. Mbinu hiyo ni ya matumizi ya mitandao ya kijamii katika kufanya biashara ya bidhaa mbalimbali.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe Jumapili kwa wiki kadhaa, umebainisha kwamba biashara hiyo ya mtandao inaenea kwa kasi na mbinu wanayotumia ni kumzidishia mteja bidhaa aliyochagua popote alipo na kufanya muamala kwa njia ya simu bila kupewa risiti. Licha ya njia hiyo, kuna baadhi ya wafanyabiashara wanabeba bidhaa kwenye magari na kupita nyumba kwa nyumba kisha kuuza ama kwa fedha taslimu au mkopo na mteja kulipa kidogo kidogo kwa muda waliokubaliana.
Aina hii ya biashara imesababisha madhara kwa serikali kwa kukosa mapato stahiki ambayo yangetokana na kodi kwa kuuza bidhaa hizo. Baadhi ya wananchi waliouziwa bidhaa hizo wamekiri kwamba wanapofikishiwa bidhaa ofisini au nyumbani, wanatakiwa kufanya malipo kwa ‘lipa namba’ ya mtandao wa simu na matokeo yake hawapewi risiti.
Mbinu hiyo ya wafanyabiashara hao kuuza bidhaa bila kutoa risiti, serikali inakosa kiasi gani cha mapato? Mfano mfanyabiashara anauza friji kwa Sh. 1,200,000 kiasi cha kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ambacho ni asilimia 18 ni Sh. 216,000 na mashine ya kukamulia juisi ambayo inauzwa kwa Sh. 120,000 kiasi cha kodi kinachokwepwa ni Sh. 21,600.
Jambo la kujiuliza ni je, kwa biashara za namna hiyo serikali inakosa mapato kwa kiasi gani ambayo kiuhalisia, wafanyabiashara hao wanakwepa kodi inayolipwa na wananchi kwa kuwa wao ni mawakala wa TRA katika kukusanya VAT.
Wafanyabiashara hao, licha ya kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya shilingi kwa kukwepa kodi, wanajinufaisha kupitia kodi halali za Watanzania. Matokeo ya ukwepaji kodi huo ni kwamba mwananchi wa kawaida atakosa huduma bora kama vile afya akienda katika kituo cha kutolea huduma za afya cha serikali wakati mkwepaji kodi huyo akipata tatizo la afya, atakimbilia nje ya nchi kupata matibabu bora au katika hospitali binafsi nchini.
Kwa ujumla, ukwepaji kodi huu usipewe nafasi na njia pekee ya kutokomeza ni kwa wananchi kushirikiana na TRA katika kutoa taarifa kuhusu watu wa aina hii. Vyombo vya usalama na taasisi za utekelezaji wa sheria zishirikiane na TRA katika kupambana na uvunjaji huu wa sheria.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED