WAKATI dirisha dogo la usajili likiwa wazi tangu Desemba 15, mwaka huu, na klabu mbalimbali zikihaha huku na kule kusaka wachezaji kwa ajili ya kuviongozea nguvu vikosi vyao kuelekea hatua ya mzunguko wa pili Ligi Kuu Tanzania Bara, imeelezwa kuwa winga mtukutu wa zamani wa Klabu za Simba na Yanga, Benard Morrison, huenda akatua KenGold kama watatekeleza kile ambacho anakihitaji.
Aidha, Pamba Jiji nayo ipo kwenye mazungumzo na Klabu ya Napsa Stars ya Zambia kumtwaa Larry Bwalya.
Habari kutoka ndani ya Klabu ya KenGold, zinasema kuwa wamezungumza na Morrison na amekubali kujiunga na timu hiyo kama watampa mshahara wa Sh. milioni 10 kwa mwezi.
"Hivi tuko kwenye majadiliano kama tunaweza kufanya hivyo. Tutaangalia vitu vingi, bajeti na mambo mengine ya kiutawala kwani wachezaji wengi wanaoichezea timu hii mshahara wao haufiki hata nusu ya hiyo pesa, isiwe tukamchukua halafu ilete matatizo kwa wachezaji wengine.
Pamoja na yote ni mchezaji mzuri, kama atakuwa kwenye kiwango kile ambacho tunakijua, basi KenGold itatisha. Tusubiri tuone hali itakuwaje, kama yakienda sawa tutamtangaza, lakini kama mkiona kimya ujue imeshindikana," alisema mtoa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo.
Morrions raia wa Ghana, aliyechezea Yanga kwa misimu miwili tofauti na Simba, kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na FAR Rabat ya Morocco, ambayo alishindwa kuitumikia kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi.
Wakati hayo yakiendelea, Klabu ya Pamba Jiji imetajwa kuwa kwenye mazungumzo ya kumsajili kwa mkopo wa miezi sita, kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba, Bwalya.
Vyanzo zinasema kuwa mkataba huo una kipengele cha kumsajili mchezaji huyo jumla mwishoni mwa msimu iwapo itavutiwa na uwezo wake.
Kama akijiunga na klabu hiyo, hatokuwa mgeni kwenye Ligi Kuu, kwani aliichezea Simba, akijiunga nayo 2020 akitokea Power Dyanamos ya Zambia, hadi 2022 alipotimkia Amazulu FC ya Afrika Kusini na mwaka mmoja baadaye, Shekhukhune pia ya huko, kabla ya kujiunga na Napsa Stars ya nchini kwao Zambia mwanzoni mwa msimu huu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED