Simba kumaliza mwaka kileleni

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 03:39 PM Dec 29 2024
Kiungo wa Simba, Fabrice Ngoma (kulia) akiruka juu kufunga bao pekee kwa timu yake kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Singida Black Stars jana kwenye uwanja wa CCM Liti mkoani Singida. Simba ilishinda 1-0
Picha: Simba SC
Kiungo wa Simba, Fabrice Ngoma (kulia) akiruka juu kufunga bao pekee kwa timu yake kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Singida Black Stars jana kwenye uwanja wa CCM Liti mkoani Singida. Simba ilishinda 1-0

BAO lililofungwa dakika tatu kabla ya mapumziko na kiungo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Fabrice Ngoma jana liliiwezesha Simba kupata ushindi muhimu wa bao 1-0 dhidi ya Singida Black Stars katika mchezo mkali uliotawaliwa na rafu na mabavu kwenye uwanja wa Liti mkoani Singida.

Kona iliyopigwa na Jean Ahoua iliunganishwa kwa kichwa na Ngoma na kujaa nyavuni huku ukiwaacha wachezaji wa Singida Black Stars wakiongozwa na golikipa wake, Metacha Mnata kumzonga mwamuzi wa mchezo huo, Shomari Lawi wakilalamika golikipa huyo kuchezewa faulo kabla ya mfungaji kufunga.

Metacha alitokea na mpira huo wa kona kwa lengo la kwenda kuucheza lakini aliukosa na Ngoma kuukwamisha nyavuni.

Ushindi huo unaifanya Simba kujihakikishia kuongoza msimamo wa Ligi Kuu ikifikisha pointi 40 na itakaa kilele hadi mwakani, kwani hata kama Yanga ikishinda mchezo wa leo dhidi ya Fountain Gate unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa KMC Complex itafikisha pointi 39.

Ratiba ya Bodi ya Ligi inaonesha baada ya mechi za leo, michezo inayofuata itapigwa kuanzia Januari 20 mwakani.

Simba imemaliza mechi zake 15 za mzunguko wa kwanza ikikusanya jumla ya pointi hizo na kuwa kilele mwa msimamo wa Ligi Kuu, ikishinda michezo 12, sare moja na kupoteza mchezo mmoja huku ikifunga mabao 31 na wenyewe kuruhusu mabao matano.

Aidha, Simba imefanikiwa kushinda michezo yake yote ya ugenini katika mzunguko wa kwanza ambapo imecheza michezo saba na kushinda yote.

Mechi ya jana ilianza kwa matumizi makubwa ya nguvu, hasa Singida Black Stars ambao walionekana kutaka kupunguza kasi ya Simba huku mara kwa mara wakiwa wanamzonga mwamuzi, Lawi.

Simba ingeweza kujipatia bao mapema tu dakika ya saba, pale Yusuph Kagoma alipopata nafasi ya kuingia ndani ya eneo la hatari na kuachia shuti kali ambalo hata hivyo lilipanguliwa na kipa Metacha na kuzagaa langoni, huku Steven Mukwala akipishana nao.

Dakika mbili baadaye, Kibu Denis naye alipata nafasi akiwa nje kidogo ya boksi, shuti lake la mguu wa kushoto lilibabatiza mabeki wa Singida na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Kosakosa kwenye lango la Singida ziliendelea dakika 31, Kibu akimuwekea pasi ya kifua Mukwala ambaye aligeuka ghafla na kupiga shuti lililompita kipa Metacha, lakini ukatoka nje sentimeta chache.

Singida ilifanya shambulio la hatari langoni mwa Simba dakika ya 36, pale mshambuliaji wake, Elvis Rupia alipomzidi mbio mbio beki Che Fondoh Malone  lakini shuti lake lilipaa juu ya lango.

Baada ya kufungwa bao  wachezaji wa Singida walionekana kutoka mchezoni na kama wachezaji wa Simba wangekuwa watulivu wangeweza kupata mabao mawili ya haraka, dakika ya 43 na 44 ikiwemo 'tik-tak' ya Kibu ambayo ilitoka juu kidogo ya lango.

Sekunde chache kabla ya kwenda mapumziko, kipa wa Simba Moussa Camara alifanya kazi ya ziada alipodaka mpira wa kichwa kutoka kwa Rupia, akiunganisha krosi kutoka kwa Marouf Tchakei.

Kipindi cha pili wenyeji walikuja kwa kasi kwani dakika tatu baada ya kuanza kipindi cha pili, Rupia anayeongoza kwa upachikaji mabao kwenye Ligi Kuu akiwa na mabao manane, alipata nafasi ya kupiga shuti akiwa karibu na lango, lakini Camara kwa mara nyingine alifanya kazi ya ziada kuudaka mpira huo.

Timu zote zilifanya mabadiliko kipindi cha pili lakini haikuongeza wala kupunguza chochote kwenye mchezo huo.

Matokeo hayo yanaibakisha Singida Black Stars kwenye nafasi ya nne ikibakia na pointi 33 baada ya kucheza michezo 16.