RIPOTI MAALUM:-2 Shuruba utafutaji wa mkaa, ahueni ya matumizi nishati safi

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 09:29 PM Oct 25 2024
Seif akiwa kwenye Bajaji yake ambayo amejikita katiba bisahra hiyo na kuachana na kusafirisha mkaa kutoka porini kwa kutumia pikipiki.
Picha:Frank Monyo
Seif akiwa kwenye Bajaji yake ambayo amejikita katiba bisahra hiyo na kuachana na kusafirisha mkaa kutoka porini kwa kutumia pikipiki.

SEHEMU ya kwanza ya makala hii iliangazia namna mwendesha pikipiki alivyookuwa natafuta mkaa porini na kukumbwa na changamoto. Makala hii ya pili inaangazia athari za matumizi ya mkaa na suluhisho la nishati mbadala.

Endelea...…

SEIF, baada amechukua uamuzi wa kuacha kufanya kazi hiyo, sasa anawashawishi wenzake kuachana na shughuli hiyo.

Anasema kazi hiyo inaathari wa misitu, huku akiwapa mbinu kujikita katika biashara ndogo au ufugaji wa kuku wa kienyeji kama ambavyo anafanya yeye.

Anataja ushauri mwingine aliowapa ni kuunganisha nguvu na kukodisha gari na kwenda kubeba mkaa kwa sababu magari yameruhusiwa kwa kibali maalum.

"Katika kundi letu la watu 40, wapo walionisikiliza na kuachana na kazi hiyo, ingawa suala la kukodi gari limekuwa gumu kutokana na kipato kidogo au kuhamia kwenye biashara ya nishati mbadala..

"Hii niliiangalia kutokana na familia inayotufuata nyuma, kwani tunakuwa kwenye hatari kubwa sana ya kuziacha ama yatima au tegemezi kutokana na madhila ambayo tunakumbana nayo ikiwamo kifo na ulemavu wa kudumu," anasema.

Seif, kwa sasa amejikita katika biashara ya kusafirisha abiria kwa kutumia Bajaji, anasema kuwa kwa sasa anatumia muda wake kujitafutia riziki kwa kuendesha bajaji huku akiwashawishi wenzake kuachana na kazi hiyo hatarishi.

Rose Fantael, mkazi wa Mbezi Kibanda cha Mkaa, Dar es Salaam, alikuwa akitumia mkaa ambao upatikanaji wake unahusisha mbinu hatari zilizotolewa ufafanuzi na Seif, anasema alitawaliwa na imani kwamba bidhaa hiyo ni nafuu kuliko nishati ya gesi.

"Zamani nilikuwa ninaamini mkaa ni nafuu kuliko gesi, kumbe sio kweli. Nimeacha kutumia mkaa, ni muda sasa ninatumia gesi nyumbani kwangu na nimenunua jiko lake kabisa. Sasa ninapika kwa haraka na chakula kinakuwa kitamu tu," Rose anasema.

Rose anakiri kuokoa fedha nyingi zilizotumika kununua mkaa. Sasa ana faida nyingine - anatumia muda mfupi zaidi kupika kwa kutumia nishati safi (gesi).

Anabainisha kuwa awali alikuwa anatumia gunia moja la mkaa kwa mwezi mmoja, kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Ana familia ya watu wanane.

"Gunia la mkaa nilikuwa ninanunua Sh. 38,000, tunalitumia mwezi mmoja limeisha. Kwa sasa ninatumia gesi kilo 15 ninajaza kwa Sh. 50,000, ninatumia kwa miezi miwili au zaidi, ukilinganisha gharama za mkaa na gesi unaona kabisa gesi ni mkombozi," anasema.

MUUZA CHIPSI

Emmanuel Kipeta, mkazi wa Mbezi kwa Yusuph,Dar es Salaam, anasema elimu inatakiwa kutolewa kuhusu gharama ya nishati safi ya kupikia ikiwamo gesi

Kipate, ambaye ni mfanyabiashara wa kukaanga viazi (chipsi), anasema katika biashara yake hutumia mkaa na ziada ya kuni na maranda yanayotokana mbao zilizorandwa.

"Mimi kwa siku ninatumia gunia moja la mkaa hadi mawili ambayo ninanunua Sh. 33,000, hapo wakati mwingine ninanunua hadi Sh. 40,000, lakini nikiwaza kutumia gesi ninaona itakuwa gharama kubwa sana ukizingatia sokoni vitu vimepanda bei sana," anasema.

Kipate anasema anajua kutumia mkaa ni uteketezaji misitu na kama angekuwa na ufahamu kuhusu matumizi ya gesi na faida zake tangu awali, angehamia huko kwa kuwa anachokitafuta ni faida katika biashara yake.

WHO

Septemba 3, mwaka 2019, Mkurugenzi wa Idara ya Misitu wa TFS, Arjanson Mloge, alisema mahitaji makubwa ya mkaa yametengeneza soko kubwa jijini Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma na miji mingine.

Mloge anasema mkaa unaoingia Dar es Salaam ni gunia 500,000 kwa mwezi, akirejea utafiti uliofanywa na TFS kati ya Desemba, 2016 na Januari, 2017.

"Kiasi hiki hakijumuishi mkaa unaoingizwa isivyo halali na bodaboda zinazokisiwa kuwa takribani 200 kwa siku. Mikoa inayoingiza kwa wingi mkaa jijini Dar es Salaam ni Pwani, Tanga, Morogoro, Njombe (miti ya kupandwa), Lindi na Mtwara," Mloge alibainisha.

Shirika la Afya Duniani (WHO), duniani tayari limeshaonya kupitia ripoti yake ya utafiti ya mwaka 2022 kwamba, moshi unaotokana na kuni za kupikia ni mojawapo ya visababishi vikuu vya vifo vya watoto wachanga duniani, ukigharimu maisha ya watoto 500,000 wenye umri chini ya miaka mitano kila mwaka. 

Utafiti huo unachambua matumizi ya nishati hizo na kuenea kwa magonjwa ya mfumo wa upumuaji, kwa watoto hao kupitia utafiti uliofanywa katika nchi 30 zinazoendelea kutoka bara la Asia, Afrika na Amerika ya Kusini.

Utafiti ulibaini watu bilioni tatu katika nchi zinazoendelea wanategemea kuni au mkaa, kwa ajili ya kupikia.

WHO, linasema magonjwa yanayosababishwa na moshi husababisha vifo vya watu milioni 4.3 kila mwaka, vikiyapiku magonjwa ya malaria na kifua kikuu (TB).

SULUHISHO

Katika mjadala wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia, uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, aliagiza kuundwa kwa Kikosi Kazi cha Kitaifa kitakachoandaa Dira ya Kitaifa ya Nishati Safi ya Kupikia.

Lengo kuakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanahamia katika nishati safi ya kupikia ndani ya miaka 10 ijayo.

Akisema kila taasisi za umma na binafsi zinazokusanya zaidi ya watu 300, kuanzia Januari mwaka 2023 waachane na matumizi ya kuni na mkaa.

Waratibu wakuu wa Wizara ya Nishati na kamati ya mawaziri inayoandaa dira, ambazo ni: Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu).

Zingine ni: Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati, Wizara ya Madini, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Afya, pamoja na wadau wa sekta binafsi, asasi zisizokuwa za kiserikali na washirika wa maendeleo.

Mradi unatekelezwa mijini katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Mwanza, Pwani, Tanga na Tabora unafadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya (EU) kwa thamani ya Euro milioni 30.

Pia kupitia Mradi wa Umeme Vijijini (REA), inaendelea kutekeleza programu inayowezesha kupatikana nishati safi ya kupikia na katika mchango wake, REA inawezesha usambazaji na kupatikana mitungi bora ya gesi kutoka sekta binafsi.

JICHO LA KITAALAMU

Kunatajwa kuwapo athari za kiafya kwa wazalishaji na watumiaji wa mkaa kwa kuwa una kemikali ya kaboni, ambayo inapochomwa ina hatari ya kuchafua afya ya mtu aliyeko jirani, kupitia uchafu kama masizi yanayoingia na hewa kirahisi ndani ya mapafu.

Mtaalamu wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji, Dk. Elisha Osati, anasema kuni na mkaa zina kawaida ya kutoa chembe ndogo zinazoweza kupenya katika njia ya hewa, hata kusababisha athari kiafya.

Dk. Osati anafafanua kwamba, hewa ya 'kaboni monoksaidi', inayotolewa na mkaa, pia kuni, inapoingia mwilini inapenya katika damu na kuanzisha athari ya kuondoa hewa ya Oksijeni, ambayo ni muhimu kwa uhai wa mtu na ndio unakuwa mwanzo wa madhara ya muda mfupi na mrefu.

Anadokeza adha mojawapo ya kuni na mkaa kwa mtumiaji, moyo wake kushindwa kufanya kazi.

"Uchomaji wa mkaa unaweza pia kusababisha matatizo ya kupumua na hatimaye kupata maambukizi ya njia ya hewa (ARI), ugonjwa sugu wa mapafu (COPD), pumu, saratani ya mapafu au kwa wajawazito kujifungua watoto wenye uzito wa chini."

MITUNGI NAFUU

Mkurugenzi wa Taifa Gas, Hamis Ramadhan, anasema katika kuwezesha wigo mpana wa watumiaji wa nishati hiyo mbadala, ni vyema wasambazaji wake wakawezesha zikapatikana kwa gharama nafuu.

Ramadhan, katika maoni yake anaamini huo ni mbadala na wakati huo huo unaendana na kipato cha wengi, hata kuipatia sifa ya kusaidia kuhamasisha matumizi ya gesi majumbani na kwingineko.

“Mitungi ya kilo tatu sasa hivi ipo, bei yake kujaza ni Sh. 13,000 na kimsingi inapendwa na inatumiwa na watu wengi. Mitungi ya kilo mbili iko mbioni, tuna uhakika wasambazaji wenzetu wa gesi wanaliangalia hilo suala, tutakwenda mpaka pale kiwango cha chini ya kujaza kitaruhusiwa kitendaji," anahitimisha Ramadhan, ambaye taasisi yake pia ni mdau wa mstari wa mbele kuhamasisha mageuzi hayo.