Watoto walivyogeuka kitegauchumi mitaani

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:36 AM Oct 20 2024
Picha ambayo sio halisi ikiwaonesha watoto wa mtaani wakiomba msaada kwa wapita njia.
Picha: AI
Picha ambayo sio halisi ikiwaonesha watoto wa mtaani wakiomba msaada kwa wapita njia.

FIKIRIA mtoto mwenye umri wa kwenda shuleni, badala ya kuwa darasani au nyumbani akijisomea, yuko mtaani akipita mitaa kwa mtaa kuomba fedha za michango, kwa ajili ya ujenzi wa makanisa, misikiti au ununuzi wa gari la mchungaji.

Ni maisha ya kila siku ya watoto wenye umri wa kuwa shuleni, kabla au baada ya masomo kukutwa katika mitaa mbalimbali wakiwa na karatasi mkononi lenye jina la taasisi fulani, wakisimamisha watu barabarani kuomba fedha za michango.

Hayo yanafanyika wakati Sheria ya Mtoto Sura Namba 13 Toleo la 2014, Kifungu (a) namba 12, kikizuia mtu yeyote kumwajiri au kumfanyisha mtoto kazi ambazo zinaweza kuwa na madhara kwa afya, elimu, akili, mwili au kwa maendeleo ya kimaadili ya mtoto.

Kifungu hicho kikisomwa pamoja na namba 14 kuhusu adhabu, kinaeleza kuwa mtu atakayekiuka kifungu chochote katika sehemu hiyo, atakuwa ametenda kosa na atakapotiwa hatiani atalipa faini isiyozidi Sh. milioni tano au kifungo cha miezi isiyozidi sita au vyote kwa pamoja.

Katika mahojiano maalum na waandishi wa habari hii yaliyofanyika maeneo tofauti katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, baadhi ya watoto wamekiri kufanya kazi hiyo.

WATOTO WANENA

Mtoto X, mkazi wa jijini Mwanza na mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya Msingi Igelegele, anasimulia kwamba  wanapatiwa fomu za michango kanisani, ili kuchangisha fedha mitaani kwa ajili ya ujenzi wa kanisa na wakati mwingine kukiwa na shughuli zingine za kimaendeleo.

“Mara nyingi tunapewa fomu hizo wakati wa mafundisho na unapopewa huwezi kukataa kwani ni maelekezo ya mwalimu ambaye anasema ni mpango uliowekwa na uongozi wa kanisa, ili kufikia malengo ya ujenzi husika. Mara  nyingi tunazunguka wengine huchanga na wengine hukataa,” anasema.

Mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza (jina linahifadhiwa) katika Shule ya Sekondari ya Ngara, anakiri kupewa fomu ya kuchangisha kwa ajili ya kwenda kwenye maombi nje ya mkoa.

Anasema pamoja na kupewa fomu hiyo, mwalimu wao wa dini huwa anawaelekeza mahali pa kwenda kuchangisha michango hiyo ikiwa ni pamoja na kanisani, kwa ndugu zao wa karibu na rafiki.

Mwanafunzi mwingine wa kidato cha tatu shuleni hapo (jina linahifadhiwa),  anasema  alipewa fomu na mwalimu wa malezi wa dini, ili kuchangisha mtaani fedha za kongamano la kitaifa.

Anasema jukumu hilo halimwathiri kielimu kwa kuwa anatumia muda wake ipasavyo kukusanya michango na kisha kuendelea na masomo.

WAZAZI WAFUNGUKA

Kutokana na kuwapo kwa hali hiyo, baadhi ya wazazi wamesema vitendo hivyo vinatweza utu wa watoto hao kutokana na kuzunguka maeneo mbalimbali wakiomba fedha bila kujali hali yao na hatari wawapo mitaani ambako magari, bajaji na pikipiki hupita.

Mkazi wa Ihayabuyaga Magu, mkoani Mwanza, Sara Tito, ambaye pia ni msusi, anakiri katika eneo lake la kazi kupokea watoto wa namna hiyo na kwa kwa wiki hupokea wastani wa watoto watatu.

Anasema mara nyingi wanapita na fomu za michango ya sherehe za kwaya, ujenzi wa makanisa na misikiti, huku wengine wakitumwa na wanaodaiwa kuwa wazazi, kutafuta fedha za matibabu kwa watoto wenzao.

 “Saluni kwangu mara kwa mara wanapita, wengine wanahitaji michango ya mahafali na ujenzi wa makanisa. Kama juzi alipitia mtoto akiomba mchango wa mtoto kuwa yuko hospitalini anahitaji matibabu. Kwangu mimi naona si sahihi kuwatumia watoto kwenye shughuli hizi,” anasema.

Mkazi wa jijini Mwanza, Emmanuel Kido, anasema katika biashara yake ya duka, amekuwa akiwapokea watoto mara nyingi wakiomba kuchangiwa ujenzi wa misikiti, makanisa na vyumba vya madarasa na michango ya mahafali huku wakitaja baadhi ya viongozi wa maeneo husika kuwatuma wakiwa na ushahidi wa mihuri katika fomu zao.

Naye mkazi wa Mtaa wa Bariadi, Manispaa ya Kahama, Agatha Juma, anasema kuna watoto wengi mitaani wenye umri wa kwenda shuleni, lakini wanatembea na fomu za kuomba michango ya ujenzi wa makanisa, ununuzi wa gari la mchungaji na mahafali, jambo ambalo ni kudhalilisha madhehebu na utu wa watoto husika.

Anasema huenda viongozi wa madhehebu hayo hawafahamu na badala yake kunaibuka kikundi cha watu wachache ndani ya makanisa na misikiti kinawatumia watoto kujipatia fedha na kuwataka viongozi hao kuangalia namna ya kudhibiti suala hilo, lisiendelee kujitokeza katika jamii.

Mkazi wa Nyihogo, Zabroni Allex, anasema kuna wakati amekuwa huwakamata na kuwahoji wanapata wapi muda wa kwenda shuleni, kujisomea na wengi huzunguka mitaani kipindi cha mapumziko na wakati wametoka shuleni jioni.

Merania Marashi, mkazi wa Kata ya Mahina, Mwanza, anasema suala hilo linakera. Kila siku watoto wakitoka shuleni wakishakula huenda mitaani kuchangisha fedha, wengine wakidai kutumwa shuleni, makanisani na misikitini.

“Kila siku tunakemea ukatili majumbani. Lakini makanisani, misikitini huko nako  kumekuwa chanzo cha ukatili. Unapomtuma  mtoto mitaani akachangishe fedha unategemea nini?

“Kama si kutengeneza kizazi ambacho kitakuja kuwa hatari kwa taifa, maana uadilifu hautokuwapo kutokana na watoto kujua matumizi ya fedha wakiwa bado wadogo na wakati mwingine, kukutana na vishawishi huko mitaani,” anasema Marashi.

VIONGOZI WA DINI

Baadhi ya viongozi wa dini pamoja na serikali waliotafutwa kuelezea suala hilo, wanasema suala hilo sio la kiungwana na kuwakemea wanaofanya hivyo ya kuwa wanakiuka sheria ya mtoto.

 Mchungaji wa Kanisa la Anglikana, wilayani Kahama, Esron Yuda, anasema ni kosa kuwatumia watoto katika kukusanya michango ya aina yoyote mitaani na kuahidi kulisemea jambo hili kanisani hasa siku za ibada, ili kama lipo walikemee lisiendelee kujitokeza, kwani linadhalilisha imani zao.

 Shekhe wa Wilaya ya Kahama, Alhaji Omary Damka anasema, wanapohitaji michango ya kuendeleza dini huwa wanatumia kamati maalum ambazo huandaliwa, kwa ajili ya kukusanya michango na si kutumia watoto.

Anasema maendeleo yanohitaji kushirikisha jamii, lakini si kwa kutumia watoto kupita mitaani kuchangisha fedha.

“Watoto wanahitaji uangalizi katika malezi, kuhimizwa kusoma kwa ajili ya maisha ya baadaye na husaidia kutojiingiza katika vitendo viovu,” anasema.

Mwanasheria ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu (SHIHABI), Onesmo Daudi, anasema si sahihi kwa watoto kutumika kutafuta michango ya ujenzi wa makanisa na ununuzi wa magari ya wachungaji wao.

Anasema mzazi, mlezi au taasisi yoyote ya kidini hairuhusiwi kumbebesha majukumu mtoto kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2009 na endapo atabainika atachukuliwa hatua za kisheria, hivyo majukumu yanamnyima mtoto fursa ya kwenda shule kusoma.

Daudi anasema wanalaani vitendo vya namna hiyo kwa kuwa hali hiyo mara nyingi imekuwa ikijitokeza katika madhehebu yanayochipukia.

Anawasihi wenyeviti wa serikali za mitaa kuwachukulia hatua viongozi wa dini wanabainika kuwatumikisha watoto.

Ofisa Elimu Wilaya ya Ngara, James John, anasema ofisi yake haijapokea taarifa zozote za wanafunzi kushiriki katika kukusanya michango hiyo wakati wa masomo na kuwa, kama litakuwa linafanyika ni nje ya muda wa masomo wakati wa likizo au baada ya kutoka masomoni, wakiwa mikononi mwa wazazi.

John anakemea vitendo hivyo na kueleza kuwa mtoto anatakiwa kupata nafasi ya kupumzika na kutafakali aliyojifunza shuleni na siyo kushiriki katika kusambaza fomu za michango ya namna hiyo.

·        Imeandaliwa na Shaban Njia (KAHAMA), Rose Jacob (MWANZA), Neema Emmanuel (MWANZA), Vitus Audax (MWANZA), Judith Julius (NGARA)