Tanzania kuisaidia Somalia masuala ya kikodi

By Restuta James , Nipashe
Published at 02:13 PM Nov 21 2024
Mkuu wa chuo hicho, Prof. Isaya Jairo.
Picha:Restuta James
Mkuu wa chuo hicho, Prof. Isaya Jairo.

TANZANIA kupitia Chuo cha Kodi (ITA), inakusudia kuanzisha mifumo ya forodha na ya kikodi kwa nchi za Afrika, kwa kuwezesha uanzishwaji wa mamlaka za mapato katika nchi kadhaa, ikiwamo Somalia (Somaliland).

Aidha, ITA imesadia kuanzisha mamlaka za mapato katika nchi za Sudan Kusini na Comoro, huku kikijenga uwezo kwa maofisa wa forodha na kodi wa Botswana, Malawi na Swaziland.

Hayo yalielezwa jana Novemba 20, 2024 mkoani Dar es Salaam na Mkuu wa chuo hicho, Prof. Isaya Jairo, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mahafali ya 17 ya chuo hicho, yatakayofanyika kesho. Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba.

Alisema katika nchi ya Sudan Kusini, ITA imefundisha wanafunzi wengi kutoka nchi hiyo, akiwamo Naibu Waziri wake wa fedha.

“Sudan Kusini sisi ndio tuliosaidia kuanzisha mamlaka yao ya mapato, kwa kuwatengenezea sera mbalimbali za kiutawala na mpango mkakati wa miaka mitano, ambao unaenda hadi 2027,” alisema.
Alisema baada ya kuanzisha mamlaka hiyo, nchi hiyo imefanikiwa kuongeza mapato ya kodi hadi asilimia 20, kutoka asilimia tano na kupunguza utegemezi kwenye mafuta.

Kuhusu Somalia, Profesa Jairo alisema ITA itakwenda kushauri na kuanzisha mamlaka ya mapato, kama ilivyofanya Sudan Kusini.

“Tunatoa mafunzo na ushauri elekezi kwa wadau wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mamlaka zingine za Mapato Afrika. Mfano Zanzibar tumefanya sana, Sudan Kusini, Botswana na sasa tunajielekeza Somalia ambao wanajenga mamlaka zao za mapato,” alisema.

Profesa Jairo alisema kwa nchi za Swaziland na Malawi, chuo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo ya kujenga uwezo kwa maofisa forodha na kodi, kwa serikali zao kuwaleta ITA, hivyo kuiingizia nchi mapato na kuwajengea uwezo Watanzania wanaotoa mafunzo hayo.

Aidha, alisema ITA kinakusudia kuanzisha elimu masafa katika mwaka huu wa masomo, ili watu wengi zaidi wajiunge na kupata elimu ya forodha na kodi, ndani na nje ya nchi.
Alisema kupitia mpango huo, wanatarajia kupokea wanafunzi 5,000 hadi 7,000 kwa ngazi mbalimbali kuanzia astashaha hadi shahada ya uzamili.

Prof. Jairo alisema ITA kinatoa mafunzo yanayoendana na mabadiliko ya sayansi, teknolojia na uchumi, ambayo yanakidhi mahitaji ya soko la wataalamu wanaohitajika katika nyanja za forodha na kodi hapa nchini, barani Afrika na duniani. 

Kuhusu mahafali, Profesa Jairo, alisema wahitimu 417 watatunukiwa vyeti ambao 236 ni wa kiume na 181 ni wa kike.

“Wahitimu 195 watatunukiwa cheti cha uwakala wa forodha cha Afrika Mashariki (EACFFPC), 28 watatunukiwa cheti cha usimamizi wa forodha na kodi (CCTM), 61 watatunukiwa stashahada ya usimamizi wa forodha na kodi (DCTM) na 14 watatunukiwa stashahada ya uzamili katika kodi (PGDT),” alisema.