WAKALA wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), umetangaza kuja na mpango mpya wa kutoa huduma ya usafiri katika majiji ya Arusha, Tanga, Dodoma, Mbeya na Mwanza.
Mtendaji Mkuu wa DART, Dk. Athuman Kihamia, amesema serikali ina mpango wa kutoa huduma hiyo ya mabasi katika majiji yote nchini ili kukabiliana na msongamano wa watu na uhitaji wa mabasi hayo.
Dk. Kihamia alikuwa akizungumza katika Jiji la Tanga juzi, kuhusu mkataba wa miaka 12 itakaoingia wakati wowote mwezi huu; na Kampuni kutoka Falme za Kiarabu ya Emirates National Group (ENG) kwa ajili ya kuongeza wigo wa huduma za usafirishaji wa abiria jijini Dar es Salaam.
“Pia serikali ina mpango wa kutoa huduma hiyo ya mabasi katika majiji yote nchini, yakiwemo Mwanza, Arusha, Dodoma na Mbeya. Kwamba majiji ndiyo yenye msongamano wa watu; kwa hiyo yatapata huduma kama ilivyo katika Jiji la Dar es Salaam,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Kihamia, mchakato huo wa kumpata mtoa huduma bora nchini umekamilika na mtoa huduma huyo kutoka Abudhabi, ataanza kazi hiyo kwa kuongeza mabasi 177.
“Awamu itakuwa ni ya kutoka Mbagala kwenda Kivukoni, Mbagala/Gerezani na kwenda mpaka Morocco, na maeneo mengine ya mjini, ambapo miundombonu yake iko asilimia kama 98 hivi. Awamu hii itahitaji mabasi 755, mabasi yale makubwa yenye mita 18, mabasi 255 na mabasi yale ya wastani yenye mita 12, mabasi 500.
…Awamu ya tatu ni inayotoka Gongo la Mboto kwenda Gerezani, Gongo la Mboto kwenda Morocco, hadi Kivukoni na maeneo mengine ya mjini.”
DART, ni taasisi ya serikali iliyoundwa kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 120 la Mei 25, Mwaka 2007; chini ya Sheria Namba 30 ya Wakala za Serikali ya Mwaka 1997 na marekebisho yake.
Jukumu kuu la DART, ni kuanzisha na kuendesha mfumo wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka kwa Jiji la Dar es Salaam.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED