COP29-COP30: Ushiriki wa wanawake na hatima ya mapambano ya tabianchi

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 07:26 AM Dec 12 2025
COP29-COP30: Ushiriki wa wanawake na hatima ya mapambano ya tabianchi
Picha: Maktaba
COP29-COP30: Ushiriki wa wanawake na hatima ya mapambano ya tabianchi

Ukosefu wa uwiano wa kijinsia katika uongozi wa masuala ya tabianchi umeendelea kuwa ajenda nzito katika mjadala wa kimataifa, hasa ndani ya mfululizo wa Mikutano ya Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP).

Licha ya dunia kuendelea kupiga hatua katika mageuzi ya nishati safi na sera za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, ushiriki wa wanawake katika maamuzi makubwa bado ni mdogo. Hili limeweka shinikizo jipya kwa jumuiya ya kimataifa kuhakikisha usawa wa kijinsia unakuwa nguzo ya utekelezaji, si nadharia.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Uhusiano wa Tabianchi katika Tume ya Ulaya, Jan Dusík, amesisitiza kwamba usawa wa kijinsia ni msingi wa ustahimilivu wa jamii na mustakabali endelevu. Kauli yake inatokana na ukweli kwamba jitihada za tabianchi zisizozingatia jinsia huwaacha nyuma makundi muhimu yanayoweza kuchochea mabadiliko ya suluhisho la kudumu.

COP29 na COP30 na ushiriki wa wanawake

Mjadala kuhusu jinsia katika COP29 uliweka bayana changamoto moja kubwa: kukosekana kwa kasi ya utekelezaji wa maamuzi ya awali ya ujumuishaji wa wanawake. Ingawa kulikuwa na makubaliano ya kidhana kuhusu kuimarisha ushiriki wa wanawake, michakato mingi ya utekelezaji ilibaki bila mikakati na ushirikishwaji wa wanawake katika majadiliano ya ngazi za juu uliendelea kuwa mdogo.

Uwakilishi wa viongozi wanawake katika majukwaa ya maamuzi ya COP29 ulitajwa kuwa wa kiwango cha chini jambo lililoelezwa kuwa linatokana na kukosekana kwa dhamira thabiti ya utekelezaji.

Katika mkutano uliofuata, COP30 wa Belém, Brazil hali ilibadilika kwa kiasi kikubwa ukifungua ukurasa mpya wa sera za jinsia.

Mkutano huu haukuishia kutoa matamko tu; uliidhinisha mpango rasmi unaofahamika kama “Hatua za kukabili mabadiliko ya tabianchi zinazozingatia usawa wa kijinsia.” Mpango huu uliweka kwa mara ya kwanza mfumo mahsusi wa utekelezaji unaopaswa kufuatwa na nchi wanachama, ukieleza hatua za miongozo, rasilimali na uwajibikaji wa nchi katika kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika uongozi wa tabianchi.

Uwakilishi wa wanawake katika majadiliano ya ngazi ya juu uliongezeka katika COP30 ikilinganishwa na COP29 na wadau wanawake, viongozi wa mashirika ya kiraia na wataalamu wa jinsia walipata nafasi kubwa zaidi ya kuongoza mijadala, kutengeneza mapendekezo, na kubainisha vipaumbele vyao. Hatua hii ilionekana kama mwendelezo chanya wa jitihada za kimataifa za kuhakikisha usawa wa kijinsia hauachwi nyuma katika maamuzi ya tabianchi.

Kutoka COP29 hadi COP30

Vipaumbele vilivyopendekezwa kuhusu wanawake katika Mkutano wa COP29 vilikuwa ni pamoja na kuimarishwa kwa upatikanaji wa rasilimali, kuongeza uwakilishi katika maamuzi ya juu na kujenga uwezo wa wanawake wanaoongoza miradi ya mazingira.

Hata hivyo, changamoto kubwa ilikuwa utekelezaji kwani haukuweka utaratibu mahsusi wa kuhakikisha fedha za tabianchi zinafika kwa vikundi vya wanawake, wala haukuweka mifumo madhubuti ya uwajibikaji.

Hali hiyo ndiyo iliyofanya mkutano wa COP30 kuja na hatua za mabadiliko. Mpango uliopitishwa uliweka wazi vipaumbele vinavyotakiwa kutekelezwa, kama vile:

Mfumo wa uwazi kuhusu fedha za tabianchi unaohakikisha fedha zinawafikia moja kwa moja wanawake, hasa wale wanaosisimamia miradi ya kijamii na kimazingira.
Kuimarisha uwezo wa wanawake katika uongozi wa tabianchi kwa kutoa mafunzo, majukwaa ya ubunifu na rasilimali za utekelezaji.

Kuongeza ushiriki wa wanawake katika mipango ya kitaifa ya tabianchi, ikiwemo michakato ya kupanga na kusimamia miradi ya ustahimilivu.

Mashirika kama Global Alliance for Green and Gender Action (GAGGA) yameonya kwamba bila fedha kufika moja kwa moja kwa wanawake, mageuzi yatabaki kwenye karatasi. Hivyo, mpango wa COP30 uliongeza kipimo cha uwajibikaji ambacho kilikosekana katika COP29.

IMG-20251212-WA0001.jpg 54.58 KB


Mzigo mkubwa wa wanawake.

Wanawake, hasa katika maeneo ya vijijini, wanaendelea kubeba mzigo mkubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi. Upatikanaji mdogo wa maji safi, utegemezi wa nishati chafu kama kuni na mkaa na kupungua kwa ardhi yenye rutuba ni changamoto zinazowaathiri moja kwa moja. Ndiyo maana mjadala wa jinsia unachukuliwa kuwa si suala la haki pekee, bali pia la ufanisi wa sera.

Hayo yanathibitishwa na kauli ya Waziri wa Mazingira wa Brazil, Marina Silva ambaye amesisitiza kuwa uwekezaji kwa wanawake unaongeza kasi ya hatua madhubuti za kulinda mazingira. Mtazamo huu unakwenda sambamba na msimamo wa Mjumbe Maalumu wa Wanawake, Janja Lula da Silva, ambaye anasisitiza kwamba usawa wa kijinsia si nyongeza katika sera za tabianchi, bali ni msingi.

Sauti ya Afrika na usawa wa kijinsia

Katika bara la Afrika, ambako zaidi ya watu bilioni moja wako katika hatari ya athari za tabianchi, suala la jinsia limekuwa likipewa uzito zaidi. Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN), Dkt. Richard Muyungi, amesisitiza kuwa bara hili linatafuta suluhisho litakalolinda maisha na kuchochea maendeleo endelevu. Hapa, ushiriki wa wanawake ni muhimu kwani wao ndio msingi wa uzalishaji wa chakula, uzazi wa kijamii na usimamizi wa rasilimali.

Katika muktadha wa Tanzania, wananchi kama Justina Denis kutoka Shinyanga wanaeleza wazi kwamba mafanikio ya maazimio ya COP30 yatategemea kiwango ambacho wanawake watashirikishwa kwenye mipango ya kitaifa ya tabianchi. Kwa kuwa wanawake ndio watumiaji wakubwa wa nishati majumbani, sera zisizowahusisha haziwezi kuzaa matokeo ya kudumu.

Katika ujumla wake, COP30 imeweka rekodi kama mkutano uliobadili mwelekeo wa utekelezaji wa sera za jinsia katika mapambano ya tabianchi. Tofauti na COP29, sasa kuna dira, mpango na mifumo ambayo nchi zinatakiwa kufuata. Hatua iliyobaki ni utekelezaji na historia imeonyesha kwamba mafanikio ya tabianchi hayawezi kutenganishwa na usawa wa kijinsia.