Uzalishaji wa zao la korosho mkoani Pwani umepungua mwaka huu ikilinganishwa na msimu uliopita, ambapo kiwango cha mavuno kilikuwa kikubwa zaidi.
Meneja wa CORECU Mkoa wa Pwani, Hamis Mantawela, alitoa taarifa hiyo wakati wa mnada wa tano wa mauzo ya korosho uliofanyika wilayani Mkuranga. Mantawela alisema kuwa tofauti na mwaka jana ambapo walikuwa wamekusanya tani 20,000 kufikia mnada wa tano, mwaka huu wamekusanya tani 17,000 pekee.
“Uzalishaji umeshuka, na wenzetu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele pamoja na Bodi ya Korosho wataendelea kuchunguza chanzo cha kupungua kwa mavuno haya,” alisema.
Kuhusu malipo kwa wakulima, Mantawela alibainisha kuwa hadi sasa zaidi ya shilingi bilioni 40 zimeshalipwa. Aidha, katika mnada wa tano, tani 1,000 za korosho zimeuzwa, zikiwemo tani 850 za daraja la kwanza na tani 150 za daraja la pili.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Ikwiriri AMCOS, Kassim Mpeluye, alilalamikia baadhi ya makatibu wa vyama vya ushirika kwa kuchelewesha malipo ya wakulima na kushindwa kutoa huduma bora.
“Wapo makatibu wanaopewa mizigo wanakuwa kama wafalme; hawana muda wa kuwasikiliza wakulima. CORECU na ofisi ya mrajisi wanapaswa kutoa elimu na kuhakikisha wakulima wanaheshimiwa, kwani wao ndio wanaoiingizia taasisi hizi fedha,” alisema Mpeluye.
Mpeluye aliongeza kuwa baadhi ya mameneja na makatibu hawatoi ushirikiano tangu mnada wa kwanza, hivyo akazitaka mamlaka husika kuchukua hatua dhidi yao.
Afisa Ushirika wa Mkoa wa Pwani, Avaline Boazi, alisema Bodi ya Vyama vya Ushirika imeshindwa kusimamia makatibu wake ipasavyo, licha ya kuwaajiri wao wenyewe.
“Chama kinapopata changamoto, mrajisi anatakiwa kukagua. Akikuta kuna shida, hatua zichukuliwe kwa bodi ya chama kwa mujibu wa sheria, siyo kwa makatibu peke yao,” alisema.
Amesisitiza kuwa mchakato wa kumpata katibu unafanywa na bodi, hivyo inaposhindwa kuwajibisha watendaji wake, hatua dhidi ya wajumbe wa bodi lazima ziangaliwe kwa maslahi ya wakulima.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED