Watu watano ambao ni waendesha bodaboda wamefariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na lori lililofeli breki usiku wa kuamkia leo katika eneo la Dodoma Makulu, jijini Dodoma.
Ajali hiyo ilitokea baada ya lori, lililokuwa likishuka kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kushindwa kudhibiti mwendo na kwenda kugonga kijiwe cha bodaboda cha Amani kilichopo pembezoni mwa barabara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, amesema ajali hiyo ilitokea Desemba 11, 2025 majira ya saa 2:30 usiku. Mbali na vifo hivyo, mtu mmoja ambaye ni utingo wa lori alijeruhiwa. Ajali hiyo pia ilisababisha uharibifu wa pikipiki za madereva hao pamoja na kuvunjika kwa ukuta wa uzio wa nyumba iliyokuwa karibu na barabara.
“Eneo hilo lina mtelemko mkali, hivyo madereva wanapaswa kuendesha kwa tahadhari ili kuepusha maafa yanayoweza kuzuilika,” alisema Kamanda Hyera. Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na Tanroads, litaimarisha usalama katika eneo hilo kutokana na hatari inayojitokeza mara kwa mara.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabiri Shekimweri, akizungumza eneo la tukio, alisema watajadiliana na Tanroads kuweka matuta ili kupunguza mwendo wa magari na kupunguza ajali katika mtelemko huo hatarishi. “Inaonekana gari lilipata hitilafu na dereva kushindwa kulimudu, na hivyo kuwaparamia vijana wetu,” alisema.
Mashuhuda wa ajali hiyo pia walisema kuwa kishindo kikubwa kilisikika kabla ya kugundua kwamba vijana wa bodaboda wamepoteza maisha. “Walikuwa vijana wetu wanaotusaidia kila siku, leo tumeamkia msiba mkubwa,” alisema James Tusiime.
Waliopoteza maisha ni Ishad Jaa (25), Hafidhi Selemani (30), Adamu Juma (27), Ijumaa Ndafu (27) na Michael Mkande (26).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED