Viongozi Pwani wapanga mkakati kutimiza ahadi za siku 100 za Rais Samia

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 06:56 PM Dec 11 2025
Mkuu wa Mkoa, Abubakari Kunenge.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Mkoa, Abubakari Kunenge.

Viongozi wa taasisi za umma pamoja na sekretarieti ya Mkoa wa Pwani wamekutana katika kikao maalum cha kutathmini na kuweka mkakati wa pamoja wa utekelezaji wa ahadi za siku 100 za Rais Samia.

Kikao hicho kilioongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, kiliangazia mambo muhimu yakiwemo kukuza sekta ya viwanda ndani ya mkoa, kuboresha huduma za kijamii, na kuongeza vyanzo vya mapato ya ndani ya mkoa.

Mkuu wa Mkoa, Abubakari Kunenge, amebainisha kuwa serikali inaangalia Mkoa wa Pwani kama kitovu cha uwekezaji na imeanza kutoa kipaumbele cha kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu kama umeme, maji na gesi asilia ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.

“Tumekubaliana kuhakikisha kuwa yote ambayo Rais ameahidi katika kipindi cha siku 100 yatatekelezwa kikamilifu,” amesema Kunenge.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa mkoa kujipanga vizuri kuziba pengo la fedha zinazotumika kama misaada kwa kuongeza mapato kupitia vyanzo mbalimbali vya ndani na kuondoa vikwazo vinavyozuia ukusanyaji wa mapato hayo.

“Urasimu ukizidi unaondoa ufanisi, tunapaswa kuhakikisha vipaumbele vyetu vinazingatiwa kwa ufanisi na usahihi,” amesema Kunenge.

Katika kikao hicho, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imewatoa wito kwa mkoa wa Pwani kutoa maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda na biashara.

Meneja wa Kanda ya Mashariki wa TISEZA, Josephat Haule, amesema wawekezaji wanaoingia katika maeneo hayo wanatakiwa kuajiri angalau Watanzania 100,000 ili kuchangia ukuaji wa ajira na uchumi wa mkoa.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, wenyeviti wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya, pamoja na Wakuu wa Taasisi na vitengo mbalimbali vya mkoa wa Pwani.